Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hutubieni UNGA78 kwa Kiswahili - Katibu Mkuu EAC

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki amezungumza na Leah Mushi WA Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.
UN News
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki amezungumza na Leah Mushi WA Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hutubieni UNGA78 kwa Kiswahili - Katibu Mkuu EAC

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki amesema ili kuongeza ushawishi na kukuza lugha ya Kiswahili duniani ni vyema viongozi wa jumuiya wakazungumza lugha hiyo wakiwa katika mikutano mikubwa duniani akitolea mfano mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa au UNGA78.  

“Katika vikao vyetu vya jumuiya (EAC) tumewaomba marais pia wakija vikao kama hivi (UNGA78) wazungumze kwa lugha ya Kiswahili ndio sasa wananchi waanze kuwasikia wanasema nini lakini pia itakuwa mchango wao kuendelea kusukuma lugha ya Kiswahili iweze kwenda mbele kama lugha zingine.” Amesema Dkt. Mathuki katika mahojiano yake na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa 

Mfuko huu mahsusi umeandaliwa kutangaza jinsi tasnia ya habari inavyochangia katika kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili duniani.
UN/ Stella Vuzo
Mfuko huu mahsusi umeandaliwa kutangaza jinsi tasnia ya habari inavyochangia katika kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili duniani.

Tunasongesha Kiswahili

Dkt. Mathuki amesema tayari jumuiya hiyo imeanza kutekeleza mambo mbalimbali ya kusongesha lugha hiyo kimataifa. 

“Katika kikao cha baraza la mawaziri cha 43 kilichofanyika mwezi Machi mwaka huu 2023 tumekubaliana mambo yote tunayofanya katika jumuiya ya Afrika Mashariki lazima yawe kwa lugha ya Kiswahili na kiingereza. Tumeanza kutafuta wataalamu watusaidie kutafrisi nyaraka zote tunazofanya na ujumbe wowote tunaotoa lazima pia uwe kwa lugha ya Kiswahili.” 

Ili kusongesha zaidi lugha hiyo amesema wameanza mchakato wa kuanzisha vituo vya Kiswahili kwenye kila balozi za nchi wanachama ughaibuni ili kuvutia wageni pia watake kujifunza lugha hiyo adhimu. 

Hongera Uganda

Amlipoulizwa inakuwaje viongozi wengi wa kisiasa wanaposimama katika majukwaa ya kimataifa wanazungumza kwa kingereza Dkt Mathuki alisema hiyo ni kutokana na uzoefu wao wakuwa wanazungumza lugha ya kigeni lakini kuna juhudi zinafanyika akitolea “mfano nchini Uganda, katika baraza la mawaziri mafunzo ya lugha ya Kiswahili ni lazima.”