Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zakumbushwa kuongeza polisi wanawake

Afisa polisi wa Umoja wa Mataifa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR akiwa na ujumbe wa UN MINUSCA akiwa anafurahia huku amembeba mtoto aliye na jina kama lake
UN /Eskinder Debebe
Afisa polisi wa Umoja wa Mataifa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR akiwa na ujumbe wa UN MINUSCA akiwa anafurahia huku amembeba mtoto aliye na jina kama lake

Nchi zakumbushwa kuongeza polisi wanawake

Wanawake

Ikiwa leo ni siku ya Kimataifa ya Ushirikiano na Polisi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewatumia salamu za pongezi polisi ulimwenguni kote kwa kujitolea kwao kuhakikisha jamii inakuwa na amani, usalama na haki. 

Katika ujumbe wake kwa siku hii Guterres amewakumbusha pia upolisi unaolenga katika kusaka suluhisho za kijamii husaidia zaidi kujenga uaminifu na kuboresha usalama. 

“Kwa kutumia mbinu bora, akili, na rasilimali, vikosi vya polisi huongeza uwezo wa pamoja wa jamii  kukabiliana na uhalifu, kuhakikisha usalama na kuzuia migogoro.”

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametumia siku hii kukumbusha kanuni zinazotengemeza ushirikiano na polisi kuwa ni: - uwajibikaji, uwazi, na kuheshimu utofauti ndani ya jamii. Amesema hayo ni mambo muhimu yanayofanya kuwa na kjamii inayozingatia haki za kibinadamu. 

Kuongeza polisi wanawake

Maudhui ya mwaka huu yaaangazi majukumu ya polisi wanawake na Katibu Mkuu Guterres akaeleza  umuhimu wa polisi wanawake katika jamii na mchango wao, suala lililoungwa mkono na Bi. Ghada Waly, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC). 

"Kama nilivyosisitiza mara kwa mara: ili kufikia haki, tunahitaji wanawake zaidi katika haki. Hata hivyo uwakilishi katika vikosi vya polisi duniani kote unaendelea kuwa nyuma.”

Kulingana na takwimu rasmi zilizokusanywa na UNODC, mwaka 2021 kiwango cha wanawake ndani ya polisi kilianzia asilimia 5 hadi 46 katika nchi 52 ambazo takwimu zilipatikana, na viwango vya nchi nyingi vikisimama kati ya asilimia 15 na 20.

Bi. Wallya ameeleza ni “lazima tufanye vizuri zaidi” kwani katika baadhi ya nchi na kanda 52 zilizofanyiwa utafiti asilimia ya maafisa wa polisi wanawake ilikuwa chini ya asilimia moja. 

Wakati jitihada za kimataifa zimefanywa kuongeza uajiri na kubaki kwa wanawake katika majeshi ya polisi, maendeleo yamekuwa ya polepole, na takwimu zinaonesha kumekuwa na ongezeko la asilimia 2 tu duniani kote katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.