Skip to main content

UNPOL yaelimisha wanakijiji Darfur masuala ya haki za binadamu 

UNAMID kwa kushirikiana na Kamati ya Darfur Kaskazini kuhusu wanawake, iliandaa siku moja majadiliano ya azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake, amani na usalama Darfur Kaskazini
UNAMID/Albert González Farran
UNAMID kwa kushirikiana na Kamati ya Darfur Kaskazini kuhusu wanawake, iliandaa siku moja majadiliano ya azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake, amani na usalama Darfur Kaskazini

UNPOL yaelimisha wanakijiji Darfur masuala ya haki za binadamu 

Haki za binadamu

Ikiwa leo ni siku ya haki za binadamu duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Desemba 10, huko Khor Abeche kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan, polisi wa Umoja wa Mataifa, UNPOL kwenye ujumbe wa pamoja wa Umoja huo na Muungano wa Afrika (UNAMID) wametamatisha kampeni ya siku 16 ya kupinga ukatili dhidi ya kijinsia kwa kutoa mafunzo ya kusongesha haki za binadamu. Taarifa iliyoandaliwa na Luteni Japhet Chaula, afisa habari wa kikos cha 13 cha Tanzania huko UNAMID inasomwa hapa studio na Grace Kaneiya. 

Katika kijiji cha Nitega, jimboni Darfur nchini Sudan, polisi wa Umoja wa Mataifa kutoka eneo la Khor Abeche wakiendesha mafunzo kuhusu haki za binadamu. 

Mafunzo haya yaliyofunguliwa na mkaguzi wa polisi Melkiyor Fundi, yameendeshwa kwa lugha ya kiingereza huku mkalimani akitafsiri kwa lugha ya kiarabu ambapo washiriki, wanawake kwa wanaume wamepatiwa ufahamu wa haki za binadamu na madhara ya ukiukwaji wake. 

Wameelimishwa madhara ya utumikishaji watoto, ndoa za utotoni, mimba katika umri mdogo na umuhimu wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto shuleni ili wapate haki yao ya msingi ya elimu sambamba na usafirishaji haramu wa binadamu. 

Hapa mkufunzi akieleza kuwa katika jamii, awe mtoto, baba au mama ana eneo lake mahsusi la kuchangia na kutekeleza wajibu wake kwenye jamii. 

Halikadhalika amezungumzia ushirikiano baina ya walinda amani, polisi na jamii katika kuzuia uhalifu kijijini kupitia polisi jamii. 

Mwishoni mwa mafunzo washiriki walipatiwa vyeti. 

Miongoni mwa wahitimu ni Aisha Abdallah.. 

Bi. Abdallah ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi kijijini Nitega amesema wamejifunza mengi hasa athari za ukosefu wa elimu kwa mtoto wa kike na umuhimu wa polisi jamii na alichofurahia zaidi ni kuweza kunakili mafunzo kutoka ubaoni na hatoweza kusahau. 

Washiriki wa mafunzo hayo ya siku moja walikuwa takribani 75 wakijumuisha viongozi wa kijiji cha Nitega, maafisa na askari wa jeshi la polisi na viongozi wa dini. 

Wakati wa mafunzo haya, TANZBATT_13 ilihusika na kuimarisha ulinzi kwa msafara na kwenye eneo la mafunzo.