Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres apongeza ASEAN kwa kujenga madaraja ya maelewano duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wanahabari katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) mjini Jakarta, Indonesia.
UN Indonesia/Lufty Ferdiansyah
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wanahabari katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) mjini Jakarta, Indonesia.

Guterres apongeza ASEAN kwa kujenga madaraja ya maelewano duniani

Masuala ya UM

Mivutano ya kisiasa na kijiografia ikiendelea kushamiri duniani, ukanda wa Kusini-Mashariki mwa bara la Asia unatekeleza dhima muhimu ya kujenga madaraja ya maelewano duniani kote, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hii leo huko Jakarta, Indonesia. 

António Guterres alikuwa akizungumza mjini humo wakati akifungua mkutano wa pamoja wa nchi wanachama wa jumuiya za kusini-mashariki mwa Asia, ASEAN na Umoja wa Mataifa, UN, na kutangaza kuwa “ubia wetu ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati wowote.” 

Nchi wanachama wa ASEAN ni Brunei, Cambodia, Indonesia, Laos, Malaysia, Myanmar, Ufilipino, Singapore, Thailand, na Vietnam. 

Majaribu lukuki 

Katibu Mkuu amesema jamii ya kimataifa inakabiliwa na majaribu lukuki kuanzia dharura ya tabianchi hadi ongezeko la gharama za maisha duniani kote bila kusahau mizozo, vita, njaa, umaskini na ukosefu wa usawa. 

Huku kukiwa na hatari ya mpasuko mkuwa ambao anaona, Katibu Mkuu amesema nchi za ASEAN zinabeba dhima muhimu ya kujenga daraja la maelewano “katika dunia ambayo inazidi kuwa na makundi mengi tofauti tofauti inayohitaji taasisi thabiti za kimataifa kuambatana na mfumo huo, kwa misingi ya uwiano, mshikamano na umoja.” 

Bwana Guterres amesema anatoa shukrani kwa kundi hilo la ASEAN lenye nchi 10 kwa kasi yake ya kuunga mkono majawabu ya kimataifa. 

Kuna zaidi ya walinda amani 5,000 wa Umoja wa Mataifa kutoka nchi za ASEAN na kuna Mpango wa Kijamii wa kusongesha ukanda huo hadi mwaka 2045. 

Ametambua uthabiti wa ASEAN kwenye ukanda huo akisema unawasilisha uthabiti wa aina yake katika dunia a sasa yenye mgawanyiko. Chombo hicho kimejizatiti kwenye mazungumzo na kina uzoefu katika kuzuia mizozo mambo ambayo amesema ni mihimili muhimu katika utulivu. 

Amepongeza nchi wanachama wa ASEAN kwa juhudi zao thabiti za kidiplomasia za kuzuia mizozo kuanzia Rais ya Koera hadi bahari ya China Kusini, juhudi zinazofanywa kwa kuzingatia sheria ya kimataifa. 

Matumaini Myanmar yanayoyoma 

Bwana Guterres hakumung’unya maneno alipokuwa anazungumzia mzozo wa muda mrefu kwenye ukanda huo– utawala wa kijeshi nchini Myanmar ambao uliondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia na kiongozi asiyekuwa na mamlaka Aung San Suu Kyi mwezi Februari mwaka 2021. Bi. Aung na viongozi wengine bado wako gerezani. 

“Ghasia, ukatili, umaskini na ukandamizaji vinazidi kuyoyomesha matumaini ya kurejea kwa demokrasia,” amesema Guterres huku akielezea kile kinachoendelea Myanmar kuwa ni kitu kisichoendelevu. 

“Zaidi ya warohingya milioni moja bado wako Bangladesh, kwenye kambi kubwa zaidi duniani ya wakimbizi. Na cha kusikitisha, mazingira kwa wao kurejea nyumbani kwa usalama, na kwa hiari na kwa utu bado hayako. Hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa,” amesema Guterres akihutubia viongozi wa ASEAN. 

Amepaza sauti yake kushukuru mfumo wa kikanuni wa ASEAN na kusisitiza wito wa UN wa mkakati wa pamoja wa kumaliza machungu nchini kote Myanmar. 

Wito kwa utawala wa kijeshi Myanmar 

“Wito wangu kwa mamlaka Myanar ni dhahiri: achilia huru viongozi wote wanaoshikiliwa, halikadhalika wafungwa wa kisiasa; fungua milango ya kurejeshwa kwa utawala wa kidemokrasia Mynanmar.” 

Kuhusu janga la tabianchi, amelalamikia hatua za binadamu za kuharibu sayari dunia na kusema nchi za ASEAN ni miongoni mwa nchi zenye bayonuai tofauti tofauti na ambayo inakumbwa zaidi na majanga. 

Bado kuna muda wa kuchukua hatua kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi mwa mujibu wa mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015 ili hatimaye viwango vya joto vipungue, amesema Guterres. 

Mapema akizungumza na waandishi wa habari mjini Jakarta, Katibu Mkuu ameeleza bayana kuwa dunia inahitaji ushirikiano katika pande zote ili kujenga mustakabali bora kwa wote.