Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yaendelea kutoa msaada kwa manusura wa tetemeko Indonesia

Madhara ya Tsunami na tetemeko Indonesia yaliwaacha wengi bila makazi.
UNICEF/Arimacs Wilander
Madhara ya Tsunami na tetemeko Indonesia yaliwaacha wengi bila makazi.

Mashirika ya UN yaendelea kutoa msaada kwa manusura wa tetemeko Indonesia

Msaada wa Kibinadamu

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limefikisha mahema 435 ya dharura katika eneo la Balikpapan ili yagawiwe kwa familia ambazo zimeachwa bila makazi na zahma ya tetemeko na tsunami kwenye jimbo la Sulawesi.

Jumla ya mahema 1305 yanatarajia kuwasili Sulawesi katika siku chache zijazo. Akizungumzia msaada huo msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswis Charlie Yaxley amesema

 “Msaada zaidi ikiwemo mahema ya dharura , magodoro, vyandarua vya mbu, na kandili za sola vitawasili wiki chache zijazo, mahema hayo yamekabidhiwa kwa serikali ya Indonesia mjini Balikpapan , ambayo inasaidia kuyafikisha katika kisiwa cha jirani cha Sulawesi.”

Ameongeza kuwa baada ya kuiwasili Sulawesi msaada huo utasambazwa na washirika wa UNHCR ikiwemo shirika la msalaba mwekundu la Indonesia na wakfu wa kibinadamu wa kiislam nchini humo.

Nalo shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema wafanyakazi wake wanaisaidia serikali ya Indonesia kuharakisha , kudhibiti na ugawaji wa msaada jimboni Sulawesi. Pia shirika hilo linajihusisha na masuala ya kiufundi kama kusafirisha na kuhifadhi misaada inayowasili Palu na kwenye uwanja wa Ndege wa Balikpapan kwenye kisiwa cha jirani cha Borneo.

 Shirika hilo liliweka vituo viwili katika uwanja wa ndege wa Palu mapema mwezi huu na hadi sasa vituo vingine 10 vimeshawekwa kwenye maeneo ya Palu na Donggala ili kuhakikisha usambazaji na ugawaji wa misaada kunakohitajika na limepanga kufikisha malori 40 yaliyosheheni msaada kufikia leo.