Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yatoa dola milioni 15 ili kusaidia manusura wa tetemeko Indonesia

Msichana wa miaka 15 akiokolewa kutoka katika kifusi cha nyumba yao katikati mwa mji wa Sulawesi, Indonesia.
UNICEF/Tirto.id/@Arimacswilander
Msichana wa miaka 15 akiokolewa kutoka katika kifusi cha nyumba yao katikati mwa mji wa Sulawesi, Indonesia.

CERF yatoa dola milioni 15 ili kusaidia manusura wa tetemeko Indonesia

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 15 kutoka mfuko wake wa msaada wa dharura kwa ajili ya kusaidia manusura wa tetemeko la ardhi na tsunami vilivyokumba eneo la Sulawesi nchini Indonesia tarehe 28 mwezi uliopita wa Septemba.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa dharura, OCHA,  Mark Lowcock, ametangaza msaada huo leo wakati huu ambapo imeelezwa zaidi ya nyumba 66,000 zimesambaratishwa kutokana na tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa 7.4 katika kipimo cha richa.

Bwana Lowcock amesama fedha hizo za CERF zitasaidia mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo tayari yako Indonesia kusaidia katika maeneo ya kipaumbele yaliyochaguliwa na serikali katika kufikia makumi ya maelfu ya watu.

Mathalani kusaidia vituo vya afya, kliniki na hospitali ambazo zimeharibiwa au zimezidiwa mzigo wa wagonjwa. “Wafanyakazi kutoka shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA tayari wako mjini Pula, na fedha hizo zitasaidia wao na mashirika mengine kukidhi mahitaji ya wanawake na wasichana ambao mara nyingi wanakuwa hatarini katika mazingira kama ya sasa,” amesema Bwana Lowcock.

Halikadhalika fedha zitatumia kuimarisha makazi, huduma za maji safi na kujisafi na zile za ulinzi.

Hadi sasa maelfu ya watu hawawezi kurejea kwenye makazi yao, miundombinu kama vile barabara na madaraja imesombwa wakati huu ambapo bado mitetemo inaendelea kusikika.

OCHA inasema wakati serikali ya Indonesia na waokoaji wanaendelea kufanya kazi bila kuchoka kuwasilisha misaada ya kuokoa maisha, bado mahitaji ni makubwa.

“Serikali  ya Indonesia ina uzoefu na vifaa vya kutosha vya kukabilianana majanga, lakini wakati mwingine kama ilivyo kwa mataifa mengine, msaada kutoka nje unahitajika. Kwa kuzingatia ugumu wa dharura hii, mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya misaada ya kibinadamu yanashirikiana na serikali ili kuwasilisha misaada hiyo,” amesema Bwana Lowcock.

Mfuko wa CERF ulianzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2005 kusaidia waokoaji kwenye majanga ya kibinadamu kutoa huduma za dharura.