Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 1 Mali hatarini kukabiliwa na unyafuzi – WFP/UNICEF

Mtoto aliyepoteza makazi yake anakula lishe katika kliniki huko Bawa, Mali.
© UNICEF/Tiécoura N’Daou
Mtoto aliyepoteza makazi yake anakula lishe katika kliniki huko Bawa, Mali.

Watoto milioni 1 Mali hatarini kukabiliwa na unyafuzi – WFP/UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Takribani Watoto milioni moja wenye umri wa chini ya miaka 5 nchini Mali wako hatarini kutumbukia kwenye utapiamlo  uliokithiri kutokana na mchanganyiko wa mzozo wa muda mrefu, ukimbizi wa ndani na vikwazo vya kufikisha misaada ya kibinadamu. 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo katika miji ya Bamako Mali na New York, Marekani inasema kati ya hao watoto milioni moja, watoto 200,000 wako hatarini kufa kwa njaa iwapo misaada ya kuokoa maisha haitawafikia.  

“Takribani robo ya watoto wote nchini Mali wanakabiliwa na ukosefu mkubwa au wa kati wa chakula. Wakati huo huo, kwa mara ya kwanza nchini humo, zaidi ya watu 2,500 wako hatarini kukumbwa na baa la njaa kwenye eneo la Menaka linalokabiliwa na mzozo, na nusu yao ni watoto,” imesema taarifa hiyo ya UNICEF.  

Watendaij waandamizi wa UNICEF na WFP wajionea hali halisi Mali  

Onyo hilo la UNICEF linakuja wakati maafisa waandamizi wa UNICEF na wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP wametembelea nchi hiyo wiki hii kusisitiza usaidizi wa mashirika hayo kwa wananchi wa Mali kwa ushirikiano na mamlaka za maeneo ya nchi hiyo na wadau wa kibinadamu.  

"Mali inapitia kipindi kigumu cha janga la kibinadamu na inahitaji msaada ili kuepusha janga kwa watoto ambao kwa mara nyingine tena wanalipa gharama kubwa ya janga ambalo hawajasababisha,” amesema Ted Chaiban, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF anayehusika na hatua za kibinadamu na operesheni za usambazaji wa misaada.  

Ameongeza kuwa UNICEF, WFP na wadau wamekuwepo nchini Mali wakati wa kipindi kigumu cha mapito nchini humo na wataendelea kufanya kazi kushughulikia masuala ya kibinadamu na maendeleo ali mradi huduma hizo zinahitajika. 

Mtoto anatibiwa utapiamlo katika kliniki ya kuhamishwa hamishwa katika eneo la watu waliokimbia makazi yao nchini Mali.
© UNICEF/Tiécoura N’Daou
Mtoto anatibiwa utapiamlo katika kliniki ya kuhamishwa hamishwa katika eneo la watu waliokimbia makazi yao nchini Mali.

Si wakati wa kuchagua nani asaidiwe na nani aachwe  

Kwa ujumla, takribani watoto milioni 5 nchini Mali wana uhitaji wa dharura wa misaada ya kibinadamu, mathalani afya, lishe, elimu na huduma za ulinzi.  

Idadi hiyo ni ongezeko la angalau watoto milioni 1.5 tangu mwaka 2020.  

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WP Carl Skau ambaye pia ndio Afisa Mkuu wa Operesheni amesema “ni muhimu mno kuhakikisha janga la kibinadamu nchini Mali linashughulikiwa kwa umuhimu wake. Katika wakati ambao dunia imegubikwa na mizozo, hatuna haki ya kuchagua nani ahudumiwe. Lakini tuna wajibu wa kushirikiana kuokoa na kubadili maisha.”  

Amesema ni lazima kusaidia familia zilizoko hatarini, hasa watoto na wanawake na kushirikiana na wadau kuepusha baa la njaa, ukosefu wa uhakika wa kupata chakula, utapiamlo na kujengea jamii mnepo.  

Mabadiliko ya tabianchi nayo ni ‘mwiba’  

Pamoja na mapigano na ghasia, madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika baadhi ya maeneo ya Mali, yamechochea watu kukimbia makazi yao miezi ya hivi karibuni.  

Hadi tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu wa 2023, zaidi ya watu 377,000 wamefurushwa makwao kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, na nusu yao ni watoto.  

Licha ya udharura wa kibinadamu, bado ombi la kusaidia Mali la dola milioni 751.5 limefadhiliwa kwa asilimia 21 tu.  

UNICEF na WFP wanahitaji kwa dharura dola milioni 184.4 ili kufikia watu milioni 8.8 wenye uhitaji wa dharura nchini Mali mwaka huu wa 2023 na kati yao hao, milioni 4.7 ni watoto.