Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali za kijeshi si jawabu la changamoto za uongozi – Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuhusu hali inayoendelea nchini Niger.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuhusu hali inayoendelea nchini Niger.

Serikali za kijeshi si jawabu la changamoto za uongozi – Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani kabla ya kuanza ziara yake barani Afrika, Asia na Amerika, na kusema kuwa serikali za kijeshi si suluhisho akimulika mfululizo wa mapindu ya kijeshi yaliyogubika bara la Afrika katika miezi ya hivi karibuni. 

Nchi hizo ni Gabon hivi karibuni, Burkina Faso, Niger na Mali. 

Guterres amesema “hebu nianze na maneno machache kuhusu mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi ambayo tumeshuhudia miezi ya hivi karibuni barani Afrika. Nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto za utawala. Lakini serikali za kijeshi si jawabu.”  

Amesema badala yake serikali hizo huongeza zaidi matatizo. “Haziwezi kutatua janga, bali inazidi kuyachochea.”  

Ni kwa mantiki hiyo Guterres amesihi nchi zote zilizokumbwa na mapinduzi ya kijeshi, zisonge mbele kuanzisha taasisi halal iza kidemokrasia na utawala wa kisheria.   

Ziara Afrika hadi Asia 

Guterres ametaja ziara yake kuwa inaanza kesho Ijumaa ikiwa ni kiashiria cha mwezi wa diplomasia ya kimataifa, hapa New York Marekani na duniani kote.   

“Kadri maandalizi yanavyopamba moto kwa ajili ya Wiki ya Vikao vya Ngazi ya Juu vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Nitakuwa nasafiri kwenda Kenya kushiriki mkutano wa Afrika kuhusu Tabianchi, mkutano wa ASEAN na UN wa viongozi wa serikali nan chi huko Indonesia, mkutano wa viongozi wa kundi la nchi 20 zenye uchumi (G20) huko India na hatimaye mkutano wa viongozi wa kundi la nchi 77 (G77) nchini China na Cuba,” amesema Katibu Mkuu.  

Katibu Mkuu amesema wingi wa vikao hivi vya makundi tofauti unaashiria ongezeko la mgawanyiko wa makundi duniani. Nguvu inazidi kusambaa. Nchi tofauti zinashinikiza ushawishi katika maeneo tofauti.  

Mkutano wa tabianchi Afrika utajikita katika hatua kwa tabianchi kwa eneo ambalo linalipa gharama kubwa ya dharura ambayo haijachangia. 

Mkutano wa UN-ASEAN utakuwa ni fursa ya kuongeza zaidi ushirikiano kwa dunia inayobadilika kila uchao.   

Na katika G20, nchi zenye uchumi mkubwa duniani nao wanakutana, ilhali G77 ni sauti ya nchi kusini, kundi kubwa la nchi kwenye jukwaa la kimataifa.  

“Zikiwekwa pamoja, mikutano hii ya viongozi inaonesha uhai wa jamii ya kimataifa katika ushirikiano wa kimataifa,” amesema Katibu Mkuu.  

Ameonya kuwa bila ya kuimarisha na kurekebisha mifumo ya ushirikiano wa kimataifa, kuvunjikavunjika kwa makundi hayo ni jambo lisiloepukika.   

Na iwapo vitasambaratika, mizozo nayo inaweza kuibuka.   

Katibu Mkuu amesema taasisi za ushirikiano wa kimataifa zitaendelea kuwepo kwa dhati zitakuwa zinagusa maeneo yote duniani.   

Hivyo amesema huo ndio ujumbe atakaopeleka katika mikutano yote hiyo minne.  

Afrika atamulika nini? 

Guterres amesema akiwa katika Mkutano wa Afrika kuhusu Tabianchi atamulika maeneo mawili kuhusu tabianchi.  

Mosi nchi za Afrika hazijachangia katika ongezeko la joto duniani lakini “ndio ziko mstari wa mbele zikiathirika zaidi na madhara ya tabianchi ambayo in mafuriko vimbunga na ukame. 

Pili, “serikali nyingi za Afrika zinahaha kuwekeza kwenye nishati endelevu na rejelezi wakati rasilimali nyingi za sola, upepo, maji na madini mengine zimesheheni kwenye nchi zao. Kiwango cha juu cha madeni na riba kubwa vinakwamisha uwezo wao wa kupata fecha. 

Hivyo amesema tunahitaji juhudi za kimataifa kuweka Afrika mstari wa mbele katika mapinduzi ya nishati rejelezi na safi.