Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres anaonya dhidi ya hatari ya janga la nyuklia katika ujumbe kwa kumbukumbu ya Nagasaki

Sanamu ya Amani ya kumbukumbu ya Nagasaki katika Hifadhi ya Amani nchini Japani.
UN News/Pengfei Mi
Sanamu ya Amani ya kumbukumbu ya Nagasaki katika Hifadhi ya Amani nchini Japani.

Guterres anaonya dhidi ya hatari ya janga la nyuklia katika ujumbe kwa kumbukumbu ya Nagasaki

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa nchi kujitolea tena kutokomeza silaha za nyuklia katika ujumbe wake wa kuadhimisha mwaka wa 78 wa shambulio la bomu la atomiki katika mji wa Nagasaki nchini Japan, ulioadhimishwa hii leo.

Katika taarifa yake ya kumbukumbu ya siku amesema, “Tunaomboleza wale waliouawa, ambao kumbukumbu zao hazitafifia. Tunakumbuka uharibifu wa kutisha uliofanywa juu ya jiji hili na Hiroshima. Tunaheshimu nguvu na uthabiti wa watu wa Nagasaki kujenga upya jiji lao.” 

Bwana Guterres pia alitoa pongezi kwa manusura wa milipuko ya atomiki wanaojulikana kama hibakusha akisema ushuhuda wao wenye nguvu na wa kutisha utatumika milele kama ukumbusho wa haja ya kufikia ulimwengu usio na silaha za nyuklia.

“Nimeahidi kufanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa sauti na shuhuda za hibakusha zinaendelea kusikika”.

Alitoa wito kwa vijana - viongozi wa baadaye wa dunia na watoa maamuzi – kupeleka mwenge wao mbele, akisema “hatuwezi kusahau kilichotokea hapa. Lazima tuondoe kivuli cha maangamizi ya nyuklia, mara moja na kwa wote.”

Mashindano mapya ya silaha

Licha ya masomo ya kutisha ya hatari ya vita ya mwaka 1945, Guterres amesema ubinadamu sasa unakabiliwa na mbio mpya ya umiliki wa silaha kama vile silaha za nyuklia.

Amesema kwas asa mifumo ya silaha inaboreshwa, na kuwekwa katikati ya mikakati ya usalama wa kitaifa, na kufanya vifaa hivi viweze kuua kwa haraka, usahihi zaidi wakati wa mgawanyiko na kutoaminiana kati ya nchi n anchi au ukanda.

"Hatari ya maafa ya nyuklia sasa iko katika kiwango cha juu zaidi tangu Vita Baridi," alionya.

"Katika kukabiliana na vitisho hivi, jumuiya ya kimataifa lazima izungumze kama kitu kimoja. Matumizi yoyote ya silaha za nyuklia hayakubaliki. Hatutakaa kimya huku Mataifa yenye silaha za nyuklia yakikimbilia kuunda silaha hatari zaidi.” Amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Kuimarisha juhudi za upokonyaji silaha

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kuwa upokonyaji silaha ndio kiini cha Muhtasari wake wa Sera kuhusu Ajenda Mpya ya Amani, iliyozinduliwa mwezi uliopita. Inatoa wito kwa Nchi Wanachama kujitolea tena kwa haraka kutafuta ulimwengu usio na silaha za nyuklia, na kuimarisha kanuni za kimataifa dhidi ya matumizi na kuenea kwake.

“Mataifa yanayomiliki silaha za nyuklia lazima yajitolee kutozitumia kamwe. Njia pekee ya kuondoa hatari ya nyuklia ni kuondoa silaha za nyuklia,” alisema.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi na viongozi wa dunia ili kuimarisha juhudi za kimataifa za kutokomeza silaha na kuzuia kuenea kwa silaha hizo, ikiwa ni pamoja na kupitia Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia (NPT) na Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia.