Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

“Hibakusha” ni ishara ya kile UN inasimamia kutokomeza nyuklia- Guterres

Majeruhi baada ya kukimbia moto uliotokana na bomu la atomiki lililoangushwa saa 2.15 asubuhi, walikusanyika kwenye kingo ya barabara magharibi mwa Miyuki-bashi mjini Hiroshima saa tano asubuhi ya tarehe hiyo hiyo ya shambulio 6 Agosti 1945.
UN /Yoshito Matsushige
Majeruhi baada ya kukimbia moto uliotokana na bomu la atomiki lililoangushwa saa 2.15 asubuhi, walikusanyika kwenye kingo ya barabara magharibi mwa Miyuki-bashi mjini Hiroshima saa tano asubuhi ya tarehe hiyo hiyo ya shambulio 6 Agosti 1945.

“Hibakusha” ni ishara ya kile UN inasimamia kutokomeza nyuklia- Guterres

Amani na Usalama

Miaka 76 imetimu hii leo tangu Marekani iangushe bomu la nyuklia katika mji wa Hiroshima nchini Japan na kuua makumi ya maelfu ya watu papo hapo, bado hatua za kutokomeza silaha za nyuklia zinasuasua, hivyo serikali chukueni hatua kufanikisha lengo hilo. Takwimu zinaonesha kuwa watu wengine makumi ya maelfu walifariki dunia baadaye na wengine wengi miaka iliyofuatia.

 

Katika kumbukizi ya tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma ujumbe wake kwa njia ya video, akisema ni heshima kubwa kuwasilisha ujumbe huu na kutambua harakati za manusura au kwa kijapani, hibakusha ambao wamekuwa mstari wa mbele kusaka kutokomezwa kwa matumizi ya silaha za nyuklia.

Katika ujumbe huo uliowasilishwa kwenye kumbukizi iliyofanyika katika bustani ya amani ya Hiroshima, karibu na eneo la tukio, Guterres amesema, “Hiroshima siyo tu inatambuliwa kwa janga ililoikumba. Uchechemezi wa kipekee wa manusura wa tukio hilo, ni ushahidi tosha wa mnepo wa moyo wa binadamu. Wamejitolea maisha yao kuelezea uzoefu wao na kufanya kampeni ya kuhakikisha hakuna anayekumbwa na kile walichopitia.”

Guterres amesema Umoja wa Mataifa nao uko sanjari na dira ya hibakusha ya dunia bila silaha za nyuklia. “Hili lilikuwa lengo la azimio la mkutano wa kwanza kabisa wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo lilipitishwa miezi mitano tu baada ya shambulio la Hiroshima sambamba na mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku silaha za nyuklia ambao umeanza kutekelezwa tarehe 22 mwezi Januari mwaka huu.”

Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani  ya UN, jijini New York, Marekan
UN/Jihye Shin
Tarehe 18 disemba 2015, Yasuaki Yamashita, mmoja wa manusura wa shambulio la Nagasaki wajulikanao kama Hibakusha kwa kijapan na ambaye sasa anaishi Mexico, alikuwa na mazungumzo na wafanyakazi wanatoa huduma za ziara ndani ya UN, jijini New York, Marekani

Bado nina hofu silaha za nyuklia ni tishio

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya kukosekana kwa maendeleo katika kufikia lengo la dunia bila silaha za nyuklia.

“Katika miaka ya  hivi karibuni nchi zenye silaha za nyuklia zimekuwa zinaendelea kuboresha vichwa vya nyuklia  na kuchochea mashindano ya kuwa na silaha hizo. Lakini uamuzi wa Marekani na Urusi wa kuongeza muda wa mkataba wao uitwao NEW START wenye lengo la kujadili na kudhibiti silaha, ni hatua za awali za kuelekea kupunguza hatari ya janga la nyuklia,” amesema Katibu Mkuu.

NEW START ulitiwa saini kati ya Marekani na Urusi tarehe 5 mwezi Februari mwaka 2011 wakikubaliana miaka 7 ya kiwango cha umiliki wa silaha za kimkakati za uvamizi kwa muda ambao mkataba huo unatekelezwa.  Hata hivyo baada ya mkataba kumalizika mwaka 2018, nchi hizo zimekubaliana tena kuongeza muda hadi tarehe 4 mwezi Februari mwaka 2026.

Wito kwa serikali ni upi?

Katibu Mkuu ametoa wito kwa serikali zinazomiliki silaha za nyuklia zichukue hatua za kupunguza iwe ni kitaifa au kwa ushirikiano.

Aidha nchi zitumie mkutano wa 10 wa mapitio ya mkataba wa kimataifa wa kutoeneza nyuklia, NPT kuimarisha ahadi zao za kuwa na dunia bila silaha za nyuklia.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake pamoja na yeye mwenyewe, “tutaendelea kuwajibika kufikia lengo la dunia bila silaha za nyuklia.”