Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mtu anayepaswa kununuliwa, kuuzwa au kufanywa mtumwa – Katibu Mkuu UN

Vijana wawili waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu, ambao waliokolewa kutoka kambi ya wakimbizi ya Dzaleka, wanapokea msaada katika makazi nchini Malawi.
© UNODC
Vijana wawili waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu, ambao waliokolewa kutoka kambi ya wakimbizi ya Dzaleka, wanapokea msaada katika makazi nchini Malawi.

Hakuna mtu anayepaswa kununuliwa, kuuzwa au kufanywa mtumwa – Katibu Mkuu UN

Haki za binadamu

Usafirishaji haramu wa binadamu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za kimsingi za binadamu na uhuru. Inawinda watu wasio na ulinzi na hustawi wakati wa migogoro na ukosefu wa utulivu. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake kuhusu Siku ya Kimataifa dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu ambayo huadhimishwa kila tarehe 30 Julai.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hivi sasa, huku kukiwa na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, majanga ya tabianchi yanayozidi kuwa mabaya na viwango vya kuhama kwa watu visivyo na kifani, watu wengi zaidi wako katika hatari ya walanguzi wa binadamu.

"Wengi wa waathiriwa waliotambuliwa ni wanawake na watoto, ambao wengi wao wanafanyiwa ukatili mkali, kazi ya kulazimishwa, unyanyasaji wa kikatili wa kingono na unyanyasaji," Guterres amesema na kuongeza, "Na bado wafanyabiashara wanaendelea kufurahia kulindwa maovu yao. Uhalifu wao hauzingatiwi vya kutosha."

Kwa maana hii, António Guterres amependekeza kuongeza uwekezaji katika hatua za kuwatambua na kuwalinda waathiriwa, pamoja na kuimarisha utekelezaji wa sheria ili kuwawajibisha wahalifu wanaowajibisha watu walio hai. "Lazima tushiriki zaidi katika kuwasaidia waathiriwa kujenga upya maisha yao," mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema.

Takwimu za usafirishaji haramu wa binadamu

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, takriban waathirika 50,000 wa biashara haramu ya binadamu wametambuliwa na kusajiliwa katika nchi 148 duniani kote. Wanawake ni asilimia 46 yao, wasichana asilimia 19.

Unyonyaji wa kingono unasalia kuwa unyonyaji wa unaofanyika zaidi (50%) ukifuatiwa na kazi ya kulazimishwa (38%).

Ulimwenguni, mmoja kati ya watatu waliogunduliwa kuwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu ni mtoto. Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, idadi ya watoto kati ya waathiriwa waliotambuliwa imeongezeka mara tatu, wakati idadi ya wavulana imeongezeka mara tano.

Usafirishaji haramu wa binadamu ni tatizo la kimataifa ambalo halitambui mipaka ya nchi. Kwa hivyo, mara nyingi hufanyika kuwa uhalifu wa kimataifa, sawa na biashara ya kimataifa ya madawa ya kulevya na biashara ya silaha. Kwa hiyo, ili kupambana na biashara haramu ya binadamu, mbinu za kimataifa zinatakiwa kutumia ushirikiano wa kimataifa kwa njia ya kubadilishana habari na kusaidiana.