Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa mara ya kwanza IOM yatoa takwimu za waathirika na wahalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu

Teknolojia hii itaboresha uzalishaji wa takwimu za kuhifadhi faragha na kuharakisha sera inayozingatia ushahidi katika mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu
Picha: IOM 2019/ Muse Mohammed
Teknolojia hii itaboresha uzalishaji wa takwimu za kuhifadhi faragha na kuharakisha sera inayozingatia ushahidi katika mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu

Kwa mara ya kwanza IOM yatoa takwimu za waathirika na wahalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiani IOM leo kwa mara ya kwanza limetoa takwimu zinazopatikana hadharani zikiunganisha maelezo mafupi ya waathirika na wahalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu huku zikihifadhi wasifu na faragha ya manusurika.  

IOM inasema upatikanaji wa takwimu hizo umewezeshwa na teknolojia ya hali ya juu iliyotengenezwa kwa ushirikiano na utafiti wa kampuni ya teknolojia ya Microsoft na zinatoa taarifa za moja kwa moja kuhusu uhusiano kati ya waathirika na wahalifu ambapo asili ya uhusinano huo ni chanzo muhimu cha kuweza kuwasaidia waathirika na kuwashitaki wahalifu. 

Kwa kufanya takwimu hizo zipatikane kwa uwazi na kwa usalama kwa mara ya kwanza, IOM na Utafiti wa Microsoft wanalenga kushiriki mbinu hii na wahusika wa misaada ya kibinadamu duniani kote ili kuboresha utayarishaji wa takwimu za kuhifadhi faragha na kuharakisha sera zinazotegemea ushahidi katika vita dhidi ya ulanguzi wa binadamu. 

Takwimu kuhusu waathirika 

Kwa mujibu wa IOM takwimu hizo za kimataifa za waathirika na wahalifu zinapatikana kwenye kituo cha ushirikiano wa takwimu za usafirishaji haramu wa binadamu (CTDC) ambacho ni lango la kwanza la takwimu za kimataifa kuhusu biashara haramu ya binadamu.  

Mkusanyiko huu wa takwimu unajumuisha takwimu za kesi za IOM kutoka kwa zaidi ya waathirika na manusura 17,000 wa usafirishaji haramu wa binadamu waliotambuliwa katika nchi na maeneo 123, na maelezo yao ya zaidi ya wahalifu 37,000 waliofanikisha mchakato wa usafirishaji haramu wa binadamu kuanzia mwaka 2005 hadi 2022. 

Monica Goracci, mkurugenzi wa programu ya msaada na usimamizi wa uhamiaji wa IOM amesema "Kutoa takwimu kuhusu biashara haramu ya binadamu ili zipatikane kwa washikadau huku tukilinda usalama na faragha ya waathiriwa kwa njia endelevu ni muhimu katika kuandaa hatua zinazotegemea ushahidi. IOM inafurahi kufanya kazi na utafiti wa Microsoft katika kushinda changamoto ya kushirikiana takwimu za kiutawala kwa ajili ya uchambuzi." 

Vijana wawili waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu, ambao waliokolewa kutoka kambi ya wakimbizi ya Dzaleka, wanapokea msaada katika makazi nchini Malawi.
© UNODC
Vijana wawili waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu, ambao waliokolewa kutoka kambi ya wakimbizi ya Dzaleka, wanapokea msaada katika makazi nchini Malawi.

IOM na Microsoft walianza kushitrikiana 2019 

Kwa mujibu wa IOM tangu kuanza kwa “Mpango wa 2019 wa teknolojia didi ya usafirishaji haramu “, IOM na utafiti wa Microsoft wamekuwa wakifanya kazi pamoja ili kubuni na kuboresha mbinu ya kuzalisha takwimu halisia kutoka kwa rekodi nyeti za matukio ya waathirika.  

Rekodi za kesi asilia zinazotokana huhifadhi kwa usahihi maelezo ya takwimu asilia za mwathirika bila kuwakilisha waathirika halisi. 

Mwendelezo mpya wa mbinu hii, ambaco unajumuisha kiwango cha hali ya juu cha faragha huzalisha takwimu zenye dhamana za faragha zinazoweza kutambulika dhidi ya mashambulizi yoyote ya usiri, hata katika matoleo mengi ya takwimu. Mbinu hii inakuza michango endelevu na ya muda mrefu kwa msingi wa ushahidi ulioshirikishwa katika mapambano ya pamoja dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, na hivyo kufanya uwezekano wa kushirikiana takwimu zaidi na kufanya utafiti wa kina zaidi huku ukilinda faragha na uhuru wa raia hasa waathirika. 

Naye Darren Edge, mkurugenzi wa utafiti wa Microsoft na kiongozi wa mradi amesema "Kwenye kampuni ya Microsoft, tunaamini kila mtu anaweza kufaidika kwa kushirikiana kwa karibu na kwa uwazi data ili kufanya maamuzi bora na kukabiliana na baadhi ya changamoto kubwa zaidi za kijamii duniani. Kwa kulinda faragha na usalama wa waathirika kwa kutumia takwimu, na kuwawezesha watunga sera kuzitazama, kuchunguza, na kuleta maana ya takwimu hizo kupitia dashibodi shirikishi, tunaonyesha mojawapo ya njia nyingi ambazo teknolojia ya utafiti inaweza kusaidia kuratibu na kukuza juhudi za mashirika ya kupambana na biashara haramu ya binadamu duniani au mashirika yoyote yanayofanya kazi kushughulikia masuala ya haki za binadamu kwa kutumia takwimu zilizo wazi."