Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Sijakomaa kuwa mwanamke’ asema mtoto nchini Burundi manusura wa usafirishaji haramu binadamu 

Elisabeth alikuwa msichana mdogo alipobakwa na mwanamume.
© IOM 2021/Lauriane Wolfe
Elisabeth alikuwa msichana mdogo alipobakwa na mwanamume.

‘Sijakomaa kuwa mwanamke’ asema mtoto nchini Burundi manusura wa usafirishaji haramu binadamu 

Haki za binadamu

Kuelekea siku ya kimataifa ya usafiridhaji haramu binadamu, tunakwenda nchini Burundi ambako mtoto mmoja wa kike anasimulia jinsi wakati ana umri wa miaka 12 aliuzwa kwa gharama ya bia na ili kutumikishwa kingono katika nchi Jirani ya Tanzania.

 

Soundcloud

Ni Elizabeth huyu, si jina lake halisi akisema alinichukua kwa nguvu na kunirusha kitandani. Nilijaribu kukataa lakini nilishindwa na alifanya alichotaka. Nilikuwa bado mtoto, kisha akasema nakuacha, na akafungua mlango. 

Huyu ni manusura wa usafirishaji haramu ambaye alikumbwa na kisanga hicho baada ya kuahidiwa ajira. Wazazi wake walitengana akiwa bado tumboni mwa mama yake. Baba wa kambo akamkataa na kulazimika kuishi kwa babu na bibi. 

Katika mahojiano na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM nchini Burundi, anasema maisha yalikuwa magumu akaamua kuhamia kwa rafiki ambako alipata taarifa ya kuwepo kwa mwanamke anayesaidia watu kuvuka mpaka hadi Tanzania na kupata kazi. 

Nchini Tanzania alifikia mkoa wa kanda ya ziwa ambako anasema, “nilipelekwa kwenye familia moja ambayo walitambulisha kwa mwanaume mmoja ambaye niliambiwa ndiye atakuwa mume wangu, nami nikawaambia siko hapa kwa ajili ya ndoa.” 

Elizabeth anasema “walinicheka na kisha wakanikpeleka kwenye baa, sikunywa pombe. Tuliporejea usiku, wakaniambia naweza kulala kwenye chumba cha huyo mwanaume mlango wa pili. Nilipokataa walisema mtoto wao mmoja anisindikize kumbe ulikuwa mtego. Tulipofika, yule mwanaume alimwambia yule msichana amletee bia na badala yake alifunga mlango kwa nje nikabakia ndani.” 

Mwanaume huyo alimwambia hata kama utakaa kuolewa nami, tayari nimekulipia mahari ya bia usiku. 

Elizabeth anasema, “usiku ule nilipofungiwa ndani na mwanaume aliyekuwa ananibaka, nilipiga kelele lakini hakuna mtu alifanya chochote. Kila mtu alifahamu kinachoendelea na walikuwa ni ndugu zake.” 

Baada ya kumbaka na kutambua ni mtoto alimtupa nje na hakuna na pa kulala 

Alitembea nyumba kwa nyumba kusaka ajira lakini watu walihofia kwa kuwa ni mtoto na serikali ya Tanzania hairuhusu ajira kwa watoto. Hatimaye Jirani mmoja alimtambulisha kwa shirika la kiraia la KIWOHEDE linalosaidia watoto kama yeye na ndio walimuunganisha na IOM na kurejea Burundi. 

Sasa Elizabeth ana umri wa miaka 16 anapata mafunzo ya ushoni hadi atakapokuwa na umri wa kuajiriwa na anatumaini kuwa ataweza kujitegemea kwa ajira hiyo ya ushoni.