Siku ya Kupinga Usafrishaji Haramu wa Binadamu yaangazia matumizi ya teknolojia 

Mhamiaji wa Venezuela Manuela Molina (si jina lake halisi) aliahidiwa kazi nzuri nchini Trinidad, lakini dakika chache baada ya kuwasili alilazimishwa kuingia kwenye gari na kupelekwa eneo la siri.
IOM Port of Spain
Mhamiaji wa Venezuela Manuela Molina (si jina lake halisi) aliahidiwa kazi nzuri nchini Trinidad, lakini dakika chache baada ya kuwasili alilazimishwa kuingia kwenye gari na kupelekwa eneo la siri.

Siku ya Kupinga Usafrishaji Haramu wa Binadamu yaangazia matumizi ya teknolojia 

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katika ujumbe wake kuhusu Siku ya Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anakumbusha kwamba migogoro, janga la tabianchi, ukosefu wa usawa na umaskini huwaacha mamilioni ya watu katika hatari ya wahalifu wanaotumia mtandao kuwahadaa waathiriwa kwa ahadi za uwongo. 

Leo tarehe 30 mwezi huu wa Julai,na mara zote kila mwaka tarehe hii huwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, uhalifu wa kutisha na mashambulizi kamili dhidi ya haki, usalama na utu wa binadamu. 

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “matumizi na matumizi mabaya ya teknolojia” katika kutekeleza uhalifu huu unaoathiri maelfu ya wanawake, watoto na wanaume kila mwaka. Takribani kila nchi duniani imeathiriwa na biashara haramu ya binadamu kama sehemu ya kufikia, asili au njia ya kupita. 

Wengi wanadanganywa na walanguzi wa binadamu hasa kwenye mtandao. 

Guterres pia amekumbuka janga la Covid-19 ambalo liliwatenganisha watoto na vijana kutoka kwa marafiki na wenzao. “Kwa hiyo, walitumia muda mwingi wakiwa peke yao mtandaoni.” 

“Wahalifu wanachukua fursa ya dosari na udhaifu huu kufuatilia, kudhibiti na kuwanyonya waathiriwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu kuwabaini.” Anasema Guterres. 

Wasafirishaji haramu wa binadamu huficha utambulisho wao kwenye mtandao wa giza 

Kwenye mtandao, wao pia huajiri na kudanganya watu kwa ahadi za uongo za ajira. Uhalifu huu hufanyika kwenye mtandao unaoitwa mtandao wa giza, sehemu ya mtandao ambayo ni ngumu kufuatilia ambayo huwaruhusu walaghai kuficha utambulisho wao huku wakieneza nyenzo za uhalifu zinazowanyanyasa watoto kingono. 

Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kaulimbiu ya mwaka huu, ‘teknolojia, inaweza pia kuwa silaha ya kupambana na biashara haramu ya binadamu’. Hii inahitaji serikali, mashirika ya udhibiti, makampuni na mashirika ya kiraia kuja pamoja juu ya sera, sheria na ufumbuzi ambao unasaidia waathiriwa na kuwaadhibu wahalifu. 

Eneo salama kwa wote  

Mtandao yaani intaneti, kwa Guterres, unapaswa kuwa mahali salama na wazi kwa kila mtu. 

Pendekezo la Katibu Mkuu ni Mkataba wa Kidijitali wa Kimataifa unaohamasisha ulimwengu juu ya haja ya kuleta utawala bora kwenye mtandao. 

António Guterres anatoa wito kwa Siku hii ya Dunia dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu kukomesha janga hili mara moja na kwa wote. 

Biashara haramu ya binadamu iko karibu kila nchi 

Siku hii ilitangazwa na Baraza Kuu katika azimio la mwaka 2013. 

Takwimu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu, UNODC, za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa watu 50,000 waligunduliwa kuwa waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu katika nchi 148 mwaka huo. 

Nusu ya waathiriwa hawa walisafirishwa kwa madhumuni ya ngono, asilimia 38 walinyonywa katika kazi ya kulazimishwa. 

Ulimwenguni kote, mmoja kati ya watatu walioathiriwa ni mtoto. Idadi ya watoto imeongezeka mara tatu, na idadi ya wavulana imeongezeka kwa asilimia 500 katika miaka mitano iliyopita. 

Wasichana na wanawake, waathirika wakubwa 

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu António Guterres, anakariri kwamba tatizo hilo linazidi kuwa baya zaidi, hasa kwa wasichana na wanawake, ambao ndio wahanga wengi wa magendo ya binadamu duniani kote. 

Sababu nyingine zinazozidisha ni migogoro, kulazimishwa kuhama makazi yao, janga la tabianchi, ukosefu wa usawa na umaskini ambao umewaacha mamilioni ya watu katika hali ya hatari.