Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yapokea ufadhili wa kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori na usalama wa chakula

Wanyamapori wakiwa kwenye Hifadhi ya Mazingira ya Lubombo katika Ufalme wa Eswatini.
© UNESCO/Lubombo Biosphere Reserve
Wanyamapori wakiwa kwenye Hifadhi ya Mazingira ya Lubombo katika Ufalme wa Eswatini.

FAO yapokea ufadhili wa kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori na usalama wa chakula

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limekaribisha mchango wa zaidi ya dola milioni 27 uliotolewa na Muungano wa Ulaya kwa ajili ya utekelezaji wa miradi endelevu ya wanyamapori ambayo inaimarisha uhifadhi wa bioanuwai barani Afrika.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Helena Semedo miradi hiyo ina mchango mkubwa kuelekea ulimwengu endelevu na wenye usalama wa chakula kwa wote. 

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo huko Roma Italia Bi.Semedo ametaja baadhi ya maeneo ya utekelezaji kuwa ni "lishe bora" kwa kuhamasisha chakula kilicho salama, na kukuza minyororo ya thamani ya nyama za porini na za wanyama wanaofugwa, na "mazingira bora" kwa kubuni mbinu bunifu za kuboresha mazingira ambayo jamii imeyazoea, kuwajengea uwezo wa kupunguza hatari na kulinda mifumo ya ikolojia. 

Mradi huu ni awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa Usimamizi Endelevu wa Wanyamapori SWM ambapo katika awamu ya kwanza muungano wa Ulaya ulitoa takriban dola milioni 50 katika awamu ya kwanza iliyohusisha nchi za Afrika, Karibian na Pasifiki. 

“Kujenga miundo mipya ya kuhifadhi wanyamapori na kuboresha usalama wa chakula kunachukua muda,” amesema Marjeta Jager, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kurugenzi Kuu ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Muungano wa Ulaya (DG-INTPA).

Cheetahs wakiwa wamesimama wakisubiri jua kuchomoza, katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara nchini Kenya.
© UNEP/Duncan Moore
Cheetahs wakiwa wamesimama wakisubiri jua kuchomoza, katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara nchini Kenya.

Mradi utafanya nini?

Mradi wa SWM unalenga kuboresha matumizi endelevu na ya kisheria ya idadi ya wanyamapori kupitia usimamizi shirikishi wa uwindaji, uvuvi na wanyamapori. Pia inashughulikia kupunguza ulaji wa nyama pori mijini kutoka vyanzo visivyo endelevu kwa kuhimiza minyororo ya thamani ya ufugaji bora na endelevu, kuku na samaki.

FAO kwa kushirikiana na wadau wanafanya kazi katika nchi na tawala za kikanda ambako wanawafikia zaidi ya jamii 80 za wenyeji na za watu wa asili katika nchi 16.

Kupitia mradi huu wa SWM jamii zinaimarisha mbinu za kiubunifu na shirikishi zinazolengwa kuhifadhi wanyama pori, kulinda mifumo ikolojia, na kuboresha maisha ya wale wanaotegemea rasilimali hizi.

EU kuendeleza ufadhili

Jager amesema kutokana na matokeo mazuri waliyo yapata katika awamu ya kwanza ya FAO ndio maana wameona haja ya kutoa tena fedha za kutekeleza awamu ya pili. 

“Tunahitaji kuendeleza zaidi miundo iliyojaribiwa na Programu ya SWM, kusambaza na kuongeza matokeo ya Mpango, matokeo na mbinu ili kuweza kuleta matokeo chanya zaidi. Kwa sababu hii, Muungano wa Ulaya unatazamia kutoa ufadhili wa ziada ili kuendeleza Mpango wa SWM hadi Juni 2029.”

Watu wengi wa vijijini kote ulimwenguni wanaendelea kutegemea wanyamapori kwa chakula, mapato na utambulisho wao wa kitamaduni. Nyama ya mwitu ni chanzo muhimu cha protini, na mafuta.

Hata hivyo, ongezeko la mahitaji ya nyama pori, hasa katika maeneo ya mijini, linatishia idadi ya wanyamapori, uwiano wa mfumo ikolojia, na usalama wa chakula wa jamii za asili na vijijini ulimwenguni kote.