Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jinamizi la ukatili wa kingono linawaandama wanawake wanaokimbia vita Sudan: UNFPA

Kila siku katika kituo cha muda cha Bulukat, UNFPA hufanya vikao kuhusu tishio la unyanyasaji wa kijinsia. Baadhi ya watu 85 walihudhuria vikao hivi, ambapo pia walijifunza kuhusu huduma na usaidizi unaopatikana kwa walionusurika.
© UNFPA Sudan
Kila siku katika kituo cha muda cha Bulukat, UNFPA hufanya vikao kuhusu tishio la unyanyasaji wa kijinsia. Baadhi ya watu 85 walihudhuria vikao hivi, ambapo pia walijifunza kuhusu huduma na usaidizi unaopatikana kwa walionusurika.

Jinamizi la ukatili wa kingono linawaandama wanawake wanaokimbia vita Sudan: UNFPA

Wanawake

Kila siku katika kituo cha mapokezi cha Bulukat , shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA kinaendesha mafunzo kuhusu tishio la ukatili wa kijinsia na takriban watu 85 wanahudhuria ambapo wanajifunza pia kuhusu huduma na msaada uliopo kwa manusura wa ubakaji.

“Jirani yangu Rose alisafiri pamoja nami lakini alilazimika kuwaacha wbinti zake watatu mjini Khartoum. Baadaye alibaini kwamba walibakwa na genge la watu.” Anasema Martha.

Martha amewasili hivi karibuni kwenye mji wa bandari wa Malakal nchini Sudan Kusini ambao ni kituo muhimu cha watu wanaokimbia machafuko nchini Sudan na kuingia Sudan Kusini.

Zaidi ya watu 170,000 wanaorejea nyumbani na wakikimbizi wamewasili hadi sasa Malakal tangu kuzuka kwa vita nchini Sudan 15 April mwaka huu na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka endapo vita haitokoma.

Kwa mujibu wa UNFPA ukatili wa kingono umeripotiwa kuongezeka katika maeneo ya Sudan ambako mapigano yameshilka kasi lakini pia katika njia ambazo watu wanatumia kukimbia.

Balukati inahifadhi watu 5000 wanaorejea

Kituo cha usafiri cha Bulukat kando ya bandari kwa sasa kinawahifadhi watu 5,000 raia wa Sudan Kusini waliorejea kutoka Sudan.

Wanawake na wasichana katika vituo hivyo waliwaambia wafanyakazi katika makazi salama yanayoungwa mkono na UNFPA, kuwa wameshuhudia au kufanyiwa ukatili wa kijinsia uliokithiri huko Khartoum na Omdurman.

Rose aliamua kuhatarisha Maisha yake kurejea Khartoum kutafuta binti zake. Aliwakuta wawili kati yao wakiwa wamefadhaika na kufanyiwa ukatili wa kingono na aliwakimbiza hospitali. 

Baadaye angemkuta mtoto wake mdogo kando ya barabara akiwa amepoteza fahamu kutokana na kupigwa na kubakwa. Msichana huyo mdogo alikufa muda mfupi baadaye.

UNFPA inasema “Maumivu ya moyo ya Rose ni moja kati ya mengine mengi, kwani kwa mara nyingine miili ya wanawake na wasichana inakuwa uwanja wa vita katika mzozo ambao hawakushiriki kuuanzisha”.

UNFPA inafanya kazi katika majimbo ya Upper Nile, Unity na Greater Bahr el Ghazal nchini Sudan Kusini ili kuhakikisha wanaorejea na wakimbizi wanaweza kupata msaada wa afya ya ngono na uzazi na huduma za kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia. 

Wahudumu wako katika vituo vya afya, maeneo salama ya wanawake na wasichana, na kituo kikuu kimoja, ambavyo vinatoa msaada jumuishi wa matibabu, kisheria, na kisaikolojia kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia.

Ukatili usiojua mipaka

Wakiwa tayari wamejawa na hofu, tishio la kudhulumiwa zaidi linawakumba wale wanaokimbia huku wakiendelea na safari zao hatari za kufika kwenye kivuko cha mpakani. 

Wengi wanavuka Renk katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini, ama kwa barabara au kwa mashua.

UNFPA inafanya vikao vya uhamasishaji kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na kubainisha msaada unaopatikana kwa waathirika katika kituo cha usafiri cha Bulukat, ambacho karibu watu 80 huhudhuria kila siku. 

Katika kikao kimoja, Ajak alieleza kwamba vizuizi vya barabarani vilikuwa vimewekwa kwenye njia ya kuelekea Renk, huku wanawake na wanaume wakitenganishwa kutoka kwa kila mmoja wao kwa kuwa walisimamishwa. Wengi waliripoti kudhalilishwa kingono na kuibiwa pesa, chakula na mali zao.

Mara baada ya kuvuka mpaka, wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula, maji safi au aina yoyote ya vifaa vya usafi. 

Huduma za afya ni haba na pale zinapopatikana mwanamke mmoja anakumbuka kuona mjamzito anayerejea nyumbani akijifungua kwenye mashua njiani kuelekea Renk.

Nyamal, ambaye ni raia wa Sudan Kusini aliyerejea, ameliambia shirika la UNFPA, kwamba "Hata hali hii si mbaya kama ilivyokuwa Khartoum na Omdurman."

Mamilioni wanakabiliwa na hatari wakijaribu kukimbia

Kwa mujibu wa UNFPA mamilioni ya watu wanakabiliwa na hatari zinazozidi kuongezeka huku wakijaribu kutoroka Sudanili kuokoa maisha yao. 

Wengi sana wamepoteza familia na wapendwa njiani na mara nyingi mbele ya macho yao.

Wanawake wanauza nguo na mali zao ili kununua chakula, huku wengine wakitafuta kuni za kuuza jambo ambalo linawaweka katika hatari zaidi ya wanyama wanaokula wenzao wanapoingia mbali porini na mara nyingi peke yao kwenye msitu usio na watu. 

Hata wanawake wanaouza chai sokoni na kufanya kazi kwenye migahawa wako hatarini, huku kukiwa na taarifa za wafanyabiashara kuwadhulumu na kuwalazimisha kufanya ngono. 

Wanawake na watoto wengi wanalala nje kwa vile hakuna makazi rasmi, na hivyo kuongeza uwezekano wao wa kukabiliwa na dhuluma na unyanyasaji wa kingono.

Shirika hilo limeendelea kusema kwamba mgogoro huo unaweza kusababisha kuongezeka kwa mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa, ikiwa ni juu ya kiwewe cha mwili na kiakili kwa mamia ya maelfu ya watu ambao tayari wanateseka.

Kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu

UNFPA inasema mapigano yanayoendelea nchini Sudan sasa yamewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 3, huku takriban 750,000 wakitafuta hifadhi katika nchi jirani kutokana na mzozo huo, ambapo hadi sasa zaidi ya watu 175,000 wamewasili Sudan Kusini. 

Huku ghasia zikionyesha dalili chache za kupungua, idadi ya watu wanaoondoka Sudan huenda ikapita milioni 1 ifikapo Oktoba 2023.

Kuna zaidi ya wanawake na wasichana 530,500 walio katika umri wa kuzaa nchini Sudan, ambao inakadiriwa kuwa wanawake 53,000 kwa sasa ni wajawazito. Takriban 5,900 watajifungua katikati ya machafuko katika mwezi ujao. Mgogoro huo pia umewaweka wanawake na wasichana hatarini zaidi huku inakadiriwa kuwa milioni 4.2 wako katika hatari ya unyanyasaji wa kijinsia.