Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Filamu yatumika kupambana na ndoa za utotoni na ukatili mwingine wa kingono Sudan Kusini 

Kijiji nchini Sudan Kusini, barabarani kati ya Yambio na Maridi, Equatoria ya Magharibi.
UN Photo/JC McIlwaine
Kijiji nchini Sudan Kusini, barabarani kati ya Yambio na Maridi, Equatoria ya Magharibi.

Filamu yatumika kupambana na ndoa za utotoni na ukatili mwingine wa kingono Sudan Kusini 

Wanawake

Filamu mpya iliyopewa jina, “Zuia ndoa za utotoni Sudan Kusini” imeoneshwa kwa mara ya kwanza kwa wanajamii katika eneo la Yambio jimboni Equatoria Magharibi ikiwa na lengo la kupambana na unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro pamoja na ubakaji ambavyo ni matukio ya kawaida katika nchi hiyo changa zaidi ulimwenguni.  

Taarifa iliyoandaliwa na mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS inasema filamu hiyo imetengenezwa na shirika la kijamii la amani na maendeleo, COPAD ambalo linalenga kuhamasisha elimu ya wasichana. Matumaini ni kwamba filamu hii itawaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuachana na mila kama vile kuwalazimisha wasichana kuolewa wakiwa bado wana umri wadogo na badala yake waipe elimu kipaumbele. Wanajamii walioudhuria wameonekana kuguswa na filamu hii na ujumbe uliomo. Mary Mathew Zunu, mkazi wa Yambio anasema,"nimeguswa sana na filamu, hasa eneo ambalo wakati mama alipomtaka binti yake achague ndoa ya mapema wakati baba yake alitaka mtoto wao amalize masomo yake. Kwa kweli niliguswa sana wakati mwigizaji akicheza mama huyo alipogundua uamuzi wake ulikuwa na makosa, alikuwa tayari ameshachelewa.”   

Mkurugenzi wa COPAD, Silvestor Ruati anasema filamu hii ni ya kwanza katika historia ya Equatoria Magharibi kutetea kwa ujasiri na kwa hekima haki ya kila msichana kuelimika na kujitegemea kiuchumi, "tumeona wasichana wengi wanaoacha shule katika Equatoria Magharibi na Sudan Kusini kwa ujumla. Wasichana wadogo wanapewa ujauzito. Wanaacha shule katika umri mdogo wa darasa la tano. Ninachojua kupitia filamu hii, tabia nyingine zitabadilishwa kwa sababu wanapoitazama; wote ni mabinti, na kaka na dada wanaotetea haki ya msichana kwa ajili ya elimu bora. Watabadilika. ” 

Maafisa wa UNMISS kutoka ofisi ya mjini Yambio nao wamehudhuria uoneshwaji wa mara ya kwanza wa filamu hii. Moses Baggari ni Afisa msaidizi wa kitengo cha ulinzi wa mtoto katika UNMISS anasema,“kinga ni bora kuliko tiba. Ikiwa una ujumbe kama huo, basi masuala yanayohusiana na unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji mwingine, yatakoma kwa urahisi, masuala yanayohusiana na ajira na matumizi ya watoto kama askari yatakomeshwa kwa urahisi kwa sababu wanafanya kitu kingine. Masuala yanayohusu ubakaji na unyanyasaji mwingine wa kingono yatasitishwa kwa urahisi katika jamii yetu. Ulinzi wa watoto ni jukumu la pamoja. Mahali bora kwa mtoto ni nyumbani na panapofuata ni shule. Hapa ndipo watoto wanalelewa, wanajengwa kuwa raia wenye dhamana na wanaotii sheria katika nchi hii.”