Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi mapya dhidi ya bandari Ukraine ni ‘mwiba’ kwa upatikanaji chakula duniani- UN

Mfanyikazi wa Umoja wa Mataifa akichunguza uharibifu uliosababishwa na shambulio la katikati mwa jiji la Mykolaiv, Ukraine, tarehe 20 Julai.
© UNOCHA/Volodymyr Tsololo
Mfanyikazi wa Umoja wa Mataifa akichunguza uharibifu uliosababishwa na shambulio la katikati mwa jiji la Mykolaiv, Ukraine, tarehe 20 Julai.

Mashambulizi mapya dhidi ya bandari Ukraine ni ‘mwiba’ kwa upatikanaji chakula duniani- UN

Amani na Usalama

Wimbi jipya la mashambulizi yanayofanywa na Urusi dhidi ya bandari nchini Ukraine linasababisha madhara makubwa duniani ikiwemo changamoto katika uhakika wa upatikanaji wa chakula hasa katika nchi zinazoendelea. 

Hiyo ni kauli ya Mkuu wa Idara ya Siasa kwenye Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kujadili uendelezaji wa amani na usalama duniani huku likijikita katika hali inayoendelea nchini Ukraine. 

Mashambulizi mfululizo kwa siku nne haikubaliki 

Kwa mujibu wa DiCarlo, Urusi imeshambulia kwa siku nne mfulilizo imeshambulia bandari za Ukraine zilizoko Bahari Nyeusi ambazo ni Odesa, Chornomorsk na Mykolaiv, mashambulizi yakifanywa kwa makombora au ndege zisizo na rubani au drones.  

“Mashambulizi hayo yameharibu miundombinu muhimu ya bandari, ofisi na usambazaji wa nafaka na vifo vya raia,” amesema Bi.DiCarlo.  

Bi. DiCarlo amesema kitendo cha Urusi kushambulia kwa makombora bandari za Ukraine ziliko Bahari Nyeusi ni kinyume na Makubaliano ya Maelewano yaliyotiwa saini kati ya Umoja wa Mataifa na Urusi ambayo yanasema Urusi itawezesha uuzaji nje ya Ukraine wa chakula, mafuta ya alizeti na mbolea kutoka bandari za Ukraine zinazodhibitiwa.  

Amesema kama hiyo haitoshi, ushambuliaji wa miundombinu ya kiraia kunaweza kuwa kinyume na sheria za kibinadamu za kimataifa.  

Mabomu yametegwa baharini hii inatishia vyombo vya kiraia pia  

“Mwenyekiti, vitisho dhidi ya ulengaji wa vyombo vya majini vya kiraia vinavyotumia Bandari Nyeusi havikubaliki,” amesema Mkuu huyo wa Idara ya Siasa kwenye Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa “tuna hofu juu ya ripoti kwamba mabomu ya kutegwa baharini yametandazwa Bahari Nyeusi na hivyo kutishia safari za majini za vyombo vya kiraia.”  

Amesema ni vema kujiepusha na vitendo vyovyote vya kichochezi ambavyo vinaweza kusababisha hali kuwa mbay azaidi na kwamba hatari yoyote ya mzozo kusambaa kwa sababu za tukio la kijeshi Bahari Nyeusi iwe kwa bahati mbaya au kwa ajali lazima liepukwe kwa gharama yoyote ile.  

Amerejelea kuwa kitendo cha Urusi kujiondoka kwenye ushiriki wa Mkataba wa Usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi kikiambatana na mashambulizi kwa makombora dhidi ya bandari muhimu Ukraine vitazidi kufanya janga hili kuwa gumu zaidi.  

UN hatutakata tamaa hadi suluhu ipatikane 

“Katibu Mkuu amekuwa wazi: Hatuwezi kusitisha juhudi zetu za kufanikisha ufikishaji wa chakula na mbolea kwenye masoko ya dunia bila vikwazo vyovyote kutoka Ukraine na Urusi,” amesisitiza Afisa huyo mwandamizi kwenye Umoja wa Mataifa.  

Amesema njia pekee ya kukomesha janga hili ambalo linazidi kuchipua Ukraine ni kukomesha vita hii kwa kuzingatia sheria za kimataifa na kanuni zilizomo kwenye Chata ya Umoja wa Mataifa, na kwa mujibu wa maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Matumaini ya wakulima Ukraine ya kuuza mazao yao yanayoyoma - Griffiths 

Hoja ya kutaka kila hatua zichukuliwe ili kuhakikisha mashambulizi yanakoma na mkataba unaanza tena kufanya kazi kama ilivyokubaliwa imeungwa mkono na Martin Griffiths, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA ambaye akihutubia Baraza hilo amemulika suala la athari za kiutu kutokana na mashambulizi hayo na kujitoa kwa Urusi kwenye mkataba huo. 

Bwana Griffiths amesema hatua ya Urusi pamoja na mashambulizi ni pigo kubwa kwa wakulima nchini Ukraine ambao licha ya kuweko kwenye mazingira ya vita walihakikisha wanalima. 

“Wakulima nchini Ukraine wanasubiria kwa hamu mavuno ya mazao yao waliyolima katika mazingira ya vita. Licha ya hatari ya kukanyaga mabomu yaliyotegwa ardhini na vilipuzi ambavyo bado havijalipuka, sambamba na uharibifu mkubwa wa vihenge na miundombinu ya kilimo, wana hofu kwani chakula walicholima sasa kinaweza kisifikie masoko ya kimataifa,” amesema Mkuu huyo wa OCHA. 

Amesisitiza kuwa janga la kibinadamu ambalo linaendelea kuchipuka Ukraine likiwa na madhara yake duniani kote lazima likome.