Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yawakumbuka wafanyakazi wake 77 waliopoteza maisha kazini mwaka jana

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akishiriki kwenye kumbukumbu ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha wakiwa katika huduma mwaka 2022.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akishiriki kwenye kumbukumbu ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha wakiwa katika huduma mwaka 2022.

UN yawakumbuka wafanyakazi wake 77 waliopoteza maisha kazini mwaka jana

Masuala ya UM

Familia ya Umoja wa Mataifa imekutana  leo Jumatano kutoa heshima kwa wafanyikazi wake 77 waliokufa wakiwa kazini mwaka jana 2022.

"Tuko hapa kuomboleza pamoja, kukumbuka pamoja, na kutoa heshima zetu pamoja,"  amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika hafla hiyo takatifu, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Baraza la Udhamini katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.

Jamaa za wafanyakazi waliopoteza Maisha, wanachama wa jumuiya ya wanadiplomasia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kutoka duniani kote wamehudhuria hafla hiyo, ana kwa ana na mtandaoni.

Kuwaenzi wafanyakazi wenzetu wapendwa

Mwanzoni mwa hafla hiyo, Katibu Mkuu pamoja na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi na Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi wa Julai, Balozi Barbara Woodward wa Uingereza, waliwasha mshumaa unaowakilisha mwalie wa milele.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa ukimya kwa dakika moja na kishujaa kuwaenzi wafanyakazi hao huku akisema ni "kwa wenzetu wapendwa, wapendwa ambao wametoa maisha yao kwa ajili ya wengine waweze kuishi."

Majina ya wanajeshi 77, polisi na raia waliofariki dunia mwaka jana wakitumikia Umoja wa Mataifa yalisomwa wakati wa hafla hiyo.

Ujasiri na kujitolea

Bw. Guterres amesema wanaume na wanawake hawa, waliotoka nchi 36, walikuwa wafanyakazi wenzake na marafiki pia.

"Huduma yao ilijumuisha kanuni na ahadi ya Umoja wa Mataifa, kanuni ya ubinadamu wetu wa pamoja na ahadi ya kuifanyia kazi, kufanya kazi pamoja kutatua changamoto za pamoja, na kujenga ulimwengu wa amani, ustawi na haki za binadamu kwa wote," amesema.

Katibu Mkuu amesisitiza jinsi gani wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa "wanavyodumisha uhai na maono mazuri kila siku, na mara kwa mara katika hali ngumu, kama vile walinda amani na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu. Bado haijalishi jukumu lao, na hali yoyote, wale wote tunaowaenzi leo walijitolea kwa ajili ya wengine," amesema akiongeza kuwa "Ujasiri wao uliokoa maisha, kujitolea kwao kulilinda wale walio na uhitaji, na utaalam wao ulisaidia kujenga ulimwengu bora wa sasa na katika siku zijazo."

Ibada ya Ukumbusho kutoa heshima kwa wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha katika huduma yake mwaka 2022.
UN Photo/Manuel Elías
Ibada ya Ukumbusho kutoa heshima kwa wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha katika huduma yake mwaka 2022.

Kuendelea kuhuisha kumbukumbu zao

Bwana Guterres amebainisha kuwa katika ulimwengu huu uliogawanyika na hatari, dira na maadili ambayo bendera ya Umoja wa Mataifa inawakilisha ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote.

Amesisitiza dhamira ya kuendeleza utume muhimu wa Umoja wa Mataifa, kwa heshima ya wale waliotoa maisha yao katika kuhudumia shirika hili.

Katibu Mkuu amehitimisha kwa kusema kwamba "Tunaahidi kuendelea kusaidia familia. Tunajitolea kuendelea kukagua na kuboresha usalama, ulinzi na ustawi wa wafanyikazi wetu. Na tunaapa kuweka hai kumbukumbu za wenzetu waliopoteza maisha. Katika mawazo yetu, katika mioyo yetu, na katika kazi yetu ya kujenga maisha ya heshima na matumaini kwa wote,".