Hebu tuimarishe azma yetu ya pamoja na njia za kuwalinda wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakati wakifanya kazi zao bila kuchoka kwa ajili ya amani,maendeleo endelevu na vilevile haki za watu wote, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo.
kiwa ni ujumbe wake wakati wa siku ya kimataifa ya kuonyesha mshikamano na kukumbuka wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliopotea au kuuawa wakiwa kazini, Guterres amesema hii leo wafanyakazi 29 raia wa chombo hicho wako kizuizini.
Amesema wanane kati yao hao, haijulikani ni kosa gani walitenda na hakuna sababu yoyote iliyotolewa ya kushikiliwa kwao.
Bwana Guterres amesema bado wanaendelea kufuatilia visa hivyo ili waachiliwe huru.
Katibu Mkuu ameomba mataifa yote yaunge mkono mapatano ya mwaka wa 1994 kuhusu usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na washirika wake na vile vile mataifa yasisahau itifaki ya 2005 ya mapatano hayo ambayo inajumulisha wafanyakazi wa mashirika yanayotoa msaada wa kibinadamu, na wasaidizi wa masuala ya kisiasa na kimaendeleo.
Siku ya kimataifa ya mshikamano na wafanyakazi wa UN waliowekwa gerezani ama waliopotea na hawajulikani waliko, inaadhimishwa kila mwaka kukumbuka kukamatwa kwa Alec Collett, aliyekuwa mwandishi wa habari wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.