Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutaendelea kuwaenzi wenzetu waliopoteza maisha wakihudumu kupitia UN:Guterres 

Mazishi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanika nchini Mali. Luteni Kanali Carlos Moises Guillen Alfaro wa  El Salvador na Kanali Savy Sar wa Cambodia walifariki kutoka na na ugonjwa wa COVID-19.
MINUSMA/Harandane Dicko
Mazishi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yaliyofanika nchini Mali. Luteni Kanali Carlos Moises Guillen Alfaro wa El Salvador na Kanali Savy Sar wa Cambodia walifariki kutoka na na ugonjwa wa COVID-19.

Tutaendelea kuwaenzi wenzetu waliopoteza maisha wakihudumu kupitia UN:Guterres 

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa leo Alhamisi umewaenzi wafanyikazi 336 waliopoteza maisha yao wakiwa kazini mwaka 2020, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea kwa mwaka mmoja. 

Hafla ya kuwakumbuka imefanyika kwa njia ya mtandao, kutoa heshima na kuwaenzi wafanyikazi hao ambao ni raia na askari waliokufa kazini kwa sababu ya vitendo vya uasi, majanga ya asili na visa vingine. 

Kwa sababu ya janga la COVID-19 na athari zake kubwa, zikiwa ni pamoja na ufikiaji wa huduma za afya idadi hiyo hiyo pia ilijumuisha wafanyakazi waliokufa kwa COVID-19 au magonjwa mengine. 

Mwaka wa madhila tofauti na mingine 

Katika hafla hiyo ya kumbukumbu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "Mwaka 2020 haukuwa kama miaka mingine katika historia ya Umoja wa Mataifa. Ulimwengu ulikabiliwa na janga lisilo na huruma ambalo linaendelea kusababisha mateso makubwa. Mamilioni ya familia walipoteza wapendwa wao na familia ya Umoja wa Mataifa haikusalimika.” 

Katibu Mkuu alitaka kuwa na muda wa kimya kuwakumbuka wafabnyakazi waliopoteza maisha ambao majina yao yalisomwa kwa sauti wakati wa hafla hiyo ya kumbukumbu. 

Familia ya UN 

Wakiwakilisha zaidi ya mataifa 80, walitoka kila kona ya ulimwengu, na walionyesha utofauti na utajiri wa uzoefu wa Umoja wa Mataifa. 

Bwana Guterres ameongeza kuwa  "Walijitolea katika kazi zao kuendeleza maono na maadili ya Umoja wa Mataifa ya kupata amani, kuchagiza maendeleo endelevu na kuendeleza haki za binadamu". 

Patricia Nemeth, Rais wa jumuiya ya wafanyakazi ya Umoja wa Mataifa kwa upande wake ameongeza kuwa wale ambao walitoa "dhabihu kuuya maisha yao  kwa ajili ya shirika hili walifanya hivyo katika juhudi za kulinda uhuru wa walio hatarini zaidi, na kuwapa mahitaji ya kimsingi ambayo sisi sote tunayafurahia.” 

Kumbukumbu na matumaini 

Wafanyikazi waliokufa mwaka 2020 hawatasahaulika kamwe, amesema Katibu Mkuu. Pia amesisitiza ahadi ya Umoja wa Matyaifa ya kuendelea kupitia na kuboresha huduma na usalama wa wafanyakazi. 

"Walijumuisha kiini cha upendeleo wa ushirikiano wa kimataifa, watu kote ulimwenguni wakishikamana kujenga dunia bora. Kwa jina lao, tunaahidi kuendelea na kazi hiyo”, 

Ameongeza kwamba "Tunapowaenzi wenzetu wapendwa, hebu tuweke kumbukumbu zao ziwe hai kupitia kazi yetu ili kujenga maisha ya heshima, utu na matumaini kwa wote."