Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je suala la kukata hedhi lipatiwe kipaumbele pahala pa kazi? 

Wasichana wakijifunza masuala ya kuvunja ungo na hedhi kwenye darasa la wasichana pekee lililo chini ya mradi wa Umoja wa Mataifa huko Bol nchini Chad.
UN/Eskinder Debebe
Wasichana wakijifunza masuala ya kuvunja ungo na hedhi kwenye darasa la wasichana pekee lililo chini ya mradi wa Umoja wa Mataifa huko Bol nchini Chad.

Je suala la kukata hedhi lipatiwe kipaumbele pahala pa kazi? 

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na ajira duniani, ILO limeanzisha mjadala wa kuangazia iwapo suala la mwanamke kukata hedhi ni suala linalopaswa kuangaziwa pahala pa kazi baada ya utafiti uliofanyika nchini Uingereza kubaini kuwa changamoto za kiafya zitokanazo na kukatika kwa hedhi zinasababisha baadhi ya wanawake kushindwa kufanya kazi ipasavyo na wengine kuamua kuacha kazi hali inayowaathiri kiuchumi. 

Kupitia mahojiano yaliyochapishwa kwenye wavuti wa ILO, utafiti uliofanyika nchini Uingereza umebaini kuwa wanawake  zaidi ya 900,000 wamecha kazi mapema nchini humo kwa sababu ya changamoto za kukata hedhi ikiwemo kiwewe, msongo wa mawazo, ubongo kushindwa kufanya kazi ipasavyo, kukosa usingizi na mapigo ya moyo kwenda mbio. 

Utafiti unaonesha kuwa wanawake hao wanaacha kazi mapema katika umri ambao stadi zao na uzoefu vinahitajika. 

Dkt. Louise Newson, mtaalamu wa masuala ya kukatika kwa hedhi anasema, “imezoeleka kuwa hedhi kwa wanawake inakata katika umri wa miaka 50 lakini utafiti unaonesha kuwa wengine kuanzia miaka 40 na wapo wengine inakata umri wa miaka 20 na 30 na wanaanza kupata dalili za kukatika kwa hedhi.” 

Katika mahojiano hayo yaliyoendeshwa na Sophy Fisher ambaye ni Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano, ILO, Dkt. Newson amesema kwa sasa suala la kukata hedhi linaonekana ni la kifamilia lakini, “si la kifamilia tena kwa jinsi ambavyo athari zake zinakuwa za kiuchumi na hata kampuni kuanza kupoteza nguvu kazi ambayo imetumia fedha kuiendeleza.” 

Profesa Joanna Brewis kutoka Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu Huria nchini Uingereza ambaye ameandika ripoti ya utafiti huo uliogharimiwa na serikali ya Uingereza amesema kuna dalili ambazo zikiwapata wanawake kazini wanakuwa wanajisikia vibaya zaidi kwa kuwa ziko dhahiri na miongoni mwao ni kusikia joto ghafla na kutoka jasho, “na hii inashusha kiwango cha mwanamke kujiamini kwa sababu jasho linaonekana.” 

Utafiti ulibaini kuwa iwapo mwanamke atakuwa na hata dalili moja ya kukata hedhi anapokuwa na umri wa miaka 50, wakifika umri wa miaka 55 asilimia 43 wataweza kuwa wameacha kazi na asilimia 23 watapunguza saa za kazi. 

Sasa wataalamu wanataka suala la kukata hedhi liwe suala la kisera kazini ili wanawake waweze kupatiwa tiba inayotakiwa ya dawa za kuweka mizania ya homoni mwilini, tiba ambayo Dkt. Newson amesema kwa sasa ni wanawake wachache ndio wanamudu. 

Kukata hedhi kwa mwanamke ni pale mwili unapoacha kuzalisha homoni aina ya Estrojeni na Projesteroni ambazo ndio zinahusika na mzunguko wa hedhi kwa mwanamke.