Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO Bunia DRC watumia maigizo kuelimisha umma dhidi ya unyanyasaji wa kingono

Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumi
Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

MONUSCO Bunia DRC watumia maigizo kuelimisha umma dhidi ya unyanyasaji wa kingono

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ili kudhibiti unyanyasaji wa kingono ambao wakati mwingine unafanywa na baadhi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, huko jimboni Ituri katika mji wa Bunia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo – MONUSCO wanatumia ubunifu wa sanaa za maigizo ya jukwaani kuelimisha umma

Wanafunzi na wananchi wakiangalia, igizo linaendelea, mwanafunzi aliyefanyiwa unyanyasaji wa kingono hakukaa kimya amekuja katika mamlaka zinazohusika na kupokea malalamiko kueleza kilichotokea na anaambiwa amefika mahali salama na kwanza atapewa huduma ya kisaikolojia. Aliyekuwa anaongoza igizo hilo ni Debora Barugahara, yeye ni Ofisa wa MONUSCO anayehusika na tabia na nidhamu katika eneo la Bunia.  

Anasema,  “Tunafanya kuelimisha umma ili kuzuia unyanyasaji wa kingono. Tunawalenga wanafunzi wanaosoma na kuishi katika eneo la Bankoko hapa Bunia eneo ambalo ni mwenyeji wa kambi kubwa kabisa ya MONUSCO. Tumetumia maigizo ya jukwaani ili kukuza uelewa. Igizo fupi limeonesha askari wa MONUSCO na raia wakihusika katika unyanyasaji wa kiongo kwa wanafunzi. Kila mmoja alikuwa makini akifuatilia igizo lililoonesha matokeo mabaya ya unyanyasaji wa kingono. Tumehisi kwamba ujumbe umefika.” 

Marie Zaire Baguma ni Rais wa Mtandao wa Kijamii wa Malalamiko Bunia anasema,  “Tunataka jamii kuchukua kwanza umiliki wa jambo hili. Inapokuwa hivyo tunakuwa na matumaini kutakuwa na matukio machache ya unyanyasaji wa kingono.”