Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 16 wauawa Ituri, DRC wakiwemo watoto, UNICEF yalaani

Watoto wakiwa kwenye kituo chao cha kucheza ambacho ni salama. Kituo kimeanzishwa na UNICEF.
© UNICEF/Sibylle Desjardins
Watoto wakiwa kwenye kituo chao cha kucheza ambacho ni salama. Kituo kimeanzishwa na UNICEF.

Watu 16 wauawa Ituri, DRC wakiwemo watoto, UNICEF yalaani

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limelaani mauaji ya watu 16 jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kideokrasia ya Congo, DRC wakiwemo watoto 5 wa kike wenye umri wa chini ya miaka 15.
 

Mauaji hayo yaliyofanyika tarehe 3 mwezi huu wa Juni,  yametoa baada ya watu wenye silana na visu kushambulia kijiji cha Moussa kilichoko eneo la Djugu kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo la Ituri, Bunia, ambapo watu hao waliouawa walikuwa wakimbizi wa ndani waliokuwa wamerejea kwenye kijiji chao na sasa wameuawa kwa risasi na visu.
Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Edouard Beigbeder amenukuliwa katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Kinshasa akisema kuwa, “tunalaani kwa vikali shambulio hili dhidi ya watoto wasio na hatia. Tunatoa wito kwa pande husika kuheshimu haki za wanawake na watoto.”
Kutokana na shambulio hili, makumi kadhaa ya watu sasa wamekimbia eneo la Moussa na kusaka hifadhi katika vijiji vya jirani.
UNICEF inasema kuwa zaidi ya watu 300 wamefariki dunia jimboni Ituri kutokana na ghasia jimboni humo tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Kati ya mwezi Aprili na Mei pekee, UNICEF imepokea tuhuma zaidi ya 100 za ukiukwaji mkubwa wa haki dhidi ya watoto kama vile ubakaji, mauaji, ukataji viungo na mashambulizi dhidi ya shule na vituo vya afya jimboni Ituri.
Mwezi uliopita, UNICEF ilionya kuwa hali ya usalama jimboni Ituri inazidi kudorora na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa na serikali ya DRC wachukue hatua haraka kuepusha janga kubwa linaloweza kusababisha watoto kukimbia makwao, hali ambayo itawaweka watoto hatarini zaidi.
Zaidi ya watu 200,000, wengi wao wakiwa watoto wamekimbia ghasia huko Djugu, Mahagi na Irumu jimboni Ituri kuanzia mwanzoni mwa mwaka hu una wamesaka hifadhi katika jamii na maeneo ya hifadhi huko Bunia, ambayo na yenyewe yamejaa kupitia kiasi.