Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN alaani mashambulizi kwa njia ya anga nchini Sudan

Watu wanaokimbia mapigano yanayoendelea nchini Sudan wakiwasili nchini  Chad
F. Ada Affana/IOM
Watu wanaokimbia mapigano yanayoendelea nchini Sudan wakiwasili nchini Chad

Katibu Mkuu wa UN alaani mashambulizi kwa njia ya anga nchini Sudan

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres  amelaani shambulizi la anga lililotokea leo huko Omdurman nchini Sudan, ambalo limeripotiwa kuua takriban watu 22. 

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutoka jijini New York Marekani Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika wa tukio hilo na anawatakia kupona haraka wale wote waliojeruhiwa.

“Nimeshitushwa na ripoti za ghasia kubwa na majeruhi huko Darfur. Pia nina wasiwasi kuhusu ripoti za mapigano mapya katika majimbo ya Kordofan Kaskazini, Kordofan Kusini na Blue Nile. Kuna kupuuzwa kabisa kwa sheria ya kibinadamu na haki za binadamu jambo ambalo ni hatari na linasumbua.” Amesema Guterres

Katibu Mkuu huyo pia ameeleza ana wasiwasi mkubwa kwamba vita vinavyoendelea kati ya vikosi vya jeshi vimeipeleka Sudan kwenye ukingo wa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vinaweza kuyumbisha ukanda huo.

Anasisitiza wito wake kwa vikosi vya wanajeshi vya Sudan na vikosi vya Msaada wa Haraka kusitisha mapigano na kujitolea kusitisha mapigano kwa muda mrefu. 

Amehimiza pia pande zote kwenye mzozo kutii wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu na kulinda raia na kuwezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu.

Umoja wa Mataifa unaendelea kushinikiza kuunganisha juhudi za kimataifa chini ya mwamvuli unaoratibiwa na Muungano wa afrika AU na kukaribisha ushiriki mkubwa wa Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD).