Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UKIMWI Tanzania hivi sasa siyo tena hukumu ya kifo- Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia Baraza Kuu la UN
UN Video
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia Baraza Kuu la UN

UKIMWI Tanzania hivi sasa siyo tena hukumu ya kifo- Rais Samia

Afya

Tanzania imesema inaunga mkono mshikamano wa kimataifa wa kutokomeza Ukimwi duniani, kauli iliyotolewa leo na Rais wa taifa hilo Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI ulioanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya mtandao na ukumbini.
 

 

Soundcloud

Mkutano huo wa siku tatu unatathmini maendeleo yaliyofikiwa duniani katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo tangu kufanyika kwa mkutano wa ngazi hiyo mwaka 2016. 

Mkutano huu umefunguliwa na Rais wa Baraza Kuu Volkan Bozkir ambaye ametazama miongo minne iliyopita tangu mgonjwa wa kwanza wa UKIMWI akisema, “tumepiga hatua kubwa tangu mgonjwa wa kwanza wa UKIMWI. VIfo vihusianavyo na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 61 tangu maambukzi yashike kasi mwaka 2004. Tangu mkutano wa ngazi ya juu wa mwaka 2016, mataifa kadhaa yamefikia malengo yaliyowekwa ya kuchagiza hatua za kutokomeza UKIMWI, hivyo lazma tutambue mafanikio haya.”

Hata hivyo amesema kwa kiasi kikubwa malengo hayo kwenye nchi nyingi hayajafikiwa kutokana na uwekezaji mdogo ambako nchi zilizo maskini zaidi ndio zimeathirika zaidi na hazina uwezo na kwa ufafanuzi zaidi, “UKIMWI ni janga la ukosefu wa usawa, huku  Janga nalo la Corona limeongeza ‘mafuta kwenye moto.

Mwanaume akipima VVU kwenye kituo kimoja cha afya huko Odienné, nchini Côte d’Ivoire.
© UNICEF/Frank Dejongh
Mwanaume akipima VVU kwenye kituo kimoja cha afya huko Odienné, nchini Côte d’Ivoire.

Ni kwa mantiki  hiyo amesema ili kutokomeza UKIMWI mwaka 2030 ni lazima kumaliza ukosefu wa usawa katika nyanja zote.
Kwa upande wake,   Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema kuwa hatua dhidi ya UKIMWI zimeonesha kile kinachowezekana kufanikiwa iwapo kuna utashi wa kisiasa, mshikamano na sayansi na hivyo  lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 linawezekana.

Kisha viongozi mbalimbali wakaanza kutoa tathmini za vita dhidi ya UKIMWI katika nchi zao ambapo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia kwa mara ya kwanza Baraza Kuu kwa njia ya mtandao amesema, “Ukimwi siyo tena hukumu ya kifo nchini Tanzania kama ilivyokuwa miaka 38 iliyopita. Vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kutoka elfu 64 kwa mwaka 2010 hadi elfu 32 mwaka 2020. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020.”

Akasema licha ya mafanikio hayo COVID-19 inaleta mkwamo lakini hakuna janga ambalo linapaswa kupewa rasilimali  zaidi kuliko lingine na, “badala yake tunapaswa kujifunza kutokana na hatua za kukabili UKIMWI kwa kujenga jamii zenye mnepo na mifumo thabiti ya afya ambayo itakabili changamoto zijazo za kiafya na majanga.” 

Mkutano huo umepitisha azimio la kisiasa ambalo pamoja na mambo mengine linalenga kuongeza juhudi za kutokomeza UKIMWI duniani ambapo Rais Samia amesema Tanzania inaunga mkono mshikamano huo wa kimataifa.