Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu bilioni 1.8 wanaishi katika kaya zisizo na maji duniani: WHO/UNICEF

Msichana mwenye umri wa miaka 6 amebeba maji kutoka kwenye chemchemi, ambayo iko mbali na nyumba yake huko Letefoho, Hatugau, manispaa ya Ermera, Timor-Leste.
© UNICEF/Bernadino Soares
Msichana mwenye umri wa miaka 6 amebeba maji kutoka kwenye chemchemi, ambayo iko mbali na nyumba yake huko Letefoho, Hatugau, manispaa ya Ermera, Timor-Leste.

Watu bilioni 1.8 wanaishi katika kaya zisizo na maji duniani: WHO/UNICEF

Afya

Wanawake na wasichana ndio wanaobeba gharama kubwa ya mgogoro wa huduma za maji na usafi WASH imesema ripoti mpya ya uchambuzi wa kina kuhusu usawa wa kijinsia katika suala la huduma za WASH iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF na na afya duniani WHO.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, duniani kote, watu bilioni 1.8 wanaishi katika kaya zisizo na maji. 

Wanawake na wasichana wenye umri wa miaka 15 na zaidi wanawajibika hasa kwa usakaji wa maji katika kaya 7 kati ya 10, ikilinganishwa na 3 kati ya kaya 10 kwa wenzao wa kiume. 

Wasichana walio chini ya umri wa miaka 15 asilimia 7 pia wana uwezekano mkubwa wa kuchota maji kuliko wavulana walio chini ya umri wa miaka 15 ambao ni asilimia 4.

Wanawake na wasichana hutembea mwendo mrefu kusaka maji

Mashirika hayo yanasema mara nyingi, wanawake na wasichana hufanya safari ndefu kukusanya maji, wanapoteza muda katika elimu, kazi, na burudani, na kujiweka katika hatari ya kuumia kimwili na hatari wakiwa njiani.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa zaidi ya watu nusu bilioni bado wanashirikiana huduma na vifaa vya vyoo na kaya zingine, na kuhatarisha ufaragha, utu na usalama wa wanawake na wasichana.

mfano,ripoti inasema tafiti za hivi karibuni kutoka nchi 22 zinaonyesha kuwa miongoni mwa kaya zilizo na vyoo vya pamoja, wanawake na wasichana wana uwezekano mkubwa zaidi kuliko wanaume na wavulana kuhisi kutokuwa salama kutembea peke yao usiku na kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia na hatari zingine za usalama.