Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Macky Sall kutowania muhula mwingine Senegal, Katibu Mkuu UN apongeza

Rais Macky Sall wa Senegal akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Rais Macky Sall wa Senegal akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Rais Macky Sall kutowania muhula mwingine Senegal, Katibu Mkuu UN apongeza

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amepokea kwa heshima uamuzi wa Rais Macky Sall wa Senegal wa kutogombea katika uchaguzi ujao wa Rais wa nchi hiyo.  

Taarifa aliyoitoa Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq hii leo Julai 4 alasiri kwa saa za New York imesema hatua ya Rais Sall kutokogombea tena ni “kama kielelezo thabiti cha msimamo na uongozi na mfano muhimu kwa nchi yake na ulimwengu.” 

Bwana Haq ameandika kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amethibitisha uungaji mkono usioyumba wa Umoja wa Mataifa kwa Serikali na watu wa Senegal katika juhudi zao za kujumuisha utamaduni wao mahiri wa kidemokrasia na kukuza amani, utulivu na maendeleo endelevu. 

Kwa muda wa miezi kadhaa kumekuwa na maandamano nchini Senegal ya kupinga uwezekano wa Rais Sall kugombea kwa muhula wa tatu ilihali katiba ya nchi hiyo inamtaka kuongoza si zaidi ya mihula miwili.