Ajali ya helikopta CAR yaua walinda amani 3 wa Senegal, UN yazungumza

27 Septemba 2019

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, helikopta iliyokuwa imebeba walinda wanne wa Umoja wa Mataifa kutoka Senegal imeanguka leo na kusababisha vifo vya walinda amani watatu huku mmoja akijeruhiwa.

“Helikopta hiyo aina ya Mi-24, ilianguka wakati inatua kwa dharura kutokana na hali mbaya ya hewa kwenye eneo la Bouar, magharibi mwa CAR,” imesema taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, iliyotolewa leo jijini New York, Marekani  huku ikifafanua kuwa walinda amani hao wanahudumu kwenye ujumbe wa  Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA.

Taarifa hiyo inasema helikopta hiyo inatoa msaada wa usafiri wa anga kwenye operesheni zinazoendelea la MINUSCA katika jimbo la Nana-Mambéré.

Kufuatia taarifa hizo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za walinda amani  hao pamoja na serikali na wananchi wa Senegal huku akimtakia ahueni  ya haraka majeruhi.

Katibu Mkuu amesisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kusaidia serikali ya CAR katika hatua zake za kuimarisha amani.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud