Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 7.4 nchini DRC wanahitaji msaada wa kiafya: WHO

Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC
© WFP/Michael Castofas
Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC

Watu milioni 7.4 nchini DRC wanahitaji msaada wa kiafya: WHO

Afya

Baada ya miongo mitatu ya vita, mgogoro mkubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC umezorota zaidi tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Hususan sehemu ya Mashariki ya nchi hiyo inakabiliwa na ongezeko kubwa la machafuko na ukosefu wa usalama, na kuathiri vibaya afya ya watu. 

Jumla ya watu milioni 7.4 nchini DRC wanahitaji msaada wa kiafya amesema Dkt. Jorge Castilla, afisa mwandamizi wa masuala ya dharura katika shirika la afya la umoja wa Mataifa duniani WHO na meneja wa matukio nchini DRC alipozungumza na waandishi wa habari hii leo kwa njia ya video mjini Geneva Uswisi akiwa Kinshasa DRC. 

“Tangu Machi 2022, watu milioni 2.8 wamelazimika kukimbia makazi yao katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha. DRC sasa ina wakimbizi wa ndani milioni 6.3, idadi kubwa zaidi katika nchi yoyote ya Kiafrika, ambayo iko katika hatari zaidi ya milipuko ya magonjwa na utapiamlo mkali.” Limesema shirika hilo

Kwa mujibu wa WHO mfumo wa afya nchini DRC na rasilimali zilizopo ziko chini ya shinikizo kubwa kutokana na milipuko ya maradhi ya coronavirus">COVID-19, surua, polio na mpox lakini pia homa ya manjano, kipindupindu na malaria, ambayo pia yanaongezeka kutokana na majanga ya asili yanayotokea mara kwa mara na ukosefu wa huduma salama, maji na usafi wa mazingira kwa kuwa katika harakati za kukimbia.

Kutawanywa kwa watu na machafuko nchini DRC wkunachangia janga la afya
© UNICEF/Jospin Benekire
Kutawanywa kwa watu na machafuko nchini DRC wkunachangia janga la afya

Milipuko ya magonjwa

Shirika la Who linasema tangu Desemba 2022, karibu visa 25,000 vya wagonjwa wa kipindupindu na zaidi ya visa 136,000 vya wagonjwa wa surua vimeripotiwa Mashariki mwa DRC, vikijumuisha vifo 2,000 vya surua vilivyorekodiwa kufikia sasa mwaka huu. 

“Mchanganyiko wa surua na utapiamlo una madhara makubwa kiafya kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5, hivyo kuwaweka katika hatari ya kufa kwa kukosa matibabu ya kutosha.”

Mbali na ghasia hizo za kutumia silaha, mafuriko ya mapema mwaka huu yalisababisha vifo na kujeruhi mamia ya watu na kuathiri vituo 36 vya afya katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Kasai na Tshopo, na hivyo kuongeza mahitaji ya afya limeongeza kusema shirika hilo.

Pia mashambulizi dhidi ya huduma za afya yameathiri upatikanaji wa msaada wa  huduma za afya na mfumo mzima wa afya kwa sasa uko katika hali mbaya.

WHO imesema “Njaa na utapiamlo vinaongezeka, na kuwalazimu waliokimbia makazi yao kurudi mara kwa mara katika maeneo yao ya asili kukusanya rasilimali, na kuwaweka kwenye hatari zaidi na shinikizo la afya ya akili na kisaikolojia.”

Takriban watu milioni 26 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka 2023, idadi kubwa zaidi ya watu wasio na chakula duniani, na utapiamlo unaathiri sana Watoto wa chini ya umri wa miaka 5, wajawazito na mama wanaonyonyesha.

Baadhi ya uharibifu wa mazingira na mali uliofanywa na mafuriko huko Kalehe, jimboni Kivu Kusini, DRC mwezi Mei, 2023.
UN News/George Musubao
Baadhi ya uharibifu wa mazingira na mali uliofanywa na mafuriko huko Kalehe, jimboni Kivu Kusini, DRC mwezi Mei, 2023.

Msaada unaotolewa na WHO

Katika kukabiliana na changamoto hizo, WHO imeongeza msaada wake wa dharura wa afya katika majimbo ya Mashariki ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri. 

“Tunaangazia kuongeza ufikiaji wa huduma kama vile afya ya akili, unyanyasaji wa kijinsia na chanjo, tahadhari ya mapema ya magonjwa na ufuatiliaji wa kuzuia milipuko. Tunatoa dawa za kuokoa maisha na vifaa vya matibabu. Kuongeza kwenye huduma kunafuatia wito wa Umoja wa Mataifa wa kuongeza hatua za msaada wa kibinadamu Mashariki mwa DRC uliotolewa wiki iliyopita.”

 

WHO imesema kutokana na yale waliyojifunza “tunajitahidi katika kazi yetu kuzuia kikamilifu unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji wa watu walio katika mazingira magumu.”

Mwaka huu, angalau dola milioni 174 zinahitajika kutoa msaada wa dharura wa afya. 

Hata hivyo, ni dola milioni 23 tu, au asilimia 13pekee ndio zimekusanywa. 

Shirika hilo limesisitiza kwamba “Pamoja na washirika wetu, tumedhamiria kuongeza usaidizi wetu ili kuhakikisha wale wenye uhitaji nzaidi wanapata huduma za afya zinazookoa maisha. Tunatoa wito kwa wafadhili na washirika kuunganisha nguvu kwa ajili ya hatua endelevu zaidi za kiafya Mashariki mwa DRC.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP likigawa chakula katika maeneo yenye mizozo kama DRC na CAR. Sehemu ya misaada hutolewa na wadau kama USAID.
WFP/Jacques David
Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP likigawa chakula katika maeneo yenye mizozo kama DRC na CAR. Sehemu ya misaada hutolewa na wadau kama USAID.

CERF imetoa dola milioni 13 kusaidia

Kwa upande wake mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura Martin Griffths ambaye pia ni mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema janga la kibinadamu nchini DRC ni kubwa na hali ni mbaya zaidi Mashariki mwa nchi hiyo kutokana na mchanganyiko wa machafuko na majanga ya asili.

Kwa hivyo amesema “Ninatenga dola milioni 13 kutoka kwenye mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF ili kusaidia haraka jamii zilizoathirika na majanga hayo.”

Msaada huo unafanya juml a ya fedha zilizotolewa na CERF mwaka huu kwa ajili ya DRC kufikia dola milioni 35.