Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yapeleka misaada kwa waathirika wa kimbunga nchini Msumbiji

Watu wakiwa wamesimama kwenye daraja lililoharibika baada ya  Kimbunga Ana kilichoikumba Msumbiji.
© WFP
Watu wakiwa wamesimama kwenye daraja lililoharibika baada ya Kimbunga Ana kilichoikumba Msumbiji.

UNICEF yapeleka misaada kwa waathirika wa kimbunga nchini Msumbiji

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya watu 45,000 wakiwemo wanawake na watoto 23,000, huenda wakahitaji msaada wa kibinadamu baada ya kimbunga kupiga majimbo ya Nampula, Zambezia, Tete, Niassa, Sofala na Manica nchini Msumbiji tarehe 24 januari 2022. 

Shirika la Umoja wa Mataifa linalishughulikia watoto UNICEF limepeleka wafanyakazi na kuandaa vifaa vya matibabu na lishe, maji, vyoo, vifaa vya usafi, pamoja na kutenga maeneo ya kujifunzia kwa watoto na familia zilizoathiriwa na kimbuga Ana.

Athari za kimbunga Ana

Kimbunga hicho kilichoikumba nchi ya msumbiji kilisababisha mafuriko na kuharibu takriban nyumba 10,500 pamoja na miundombinu ya umma ambayo ni madaraja, shule, vituo vya afya, nyaya za umeme na mifumo ya maji.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Kupunguza na Kudhibiti Maafa ya Msumbiji (INGD), hadi kufikia Januari 26, vituo vya afya 12 na vyumba vya madarasa 346 ( katika shule 137) vimeharibiwa na kuwaacha wanafunzi 27,383 bila mahali pa kujifunzia ikiwa ni wiki moja tuu kaba ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo Jumatatu tarehe 31 Januari. 

Takwimu hizi zinatarajiwa kuongezeka wakati tathmini ikiendelea kufanyika.

Kimbunga Ana nchini Msumbiji tarehe 24 Januari 2022
© EUMETSAT
Kimbunga Ana nchini Msumbiji tarehe 24 Januari 2022

Msaada wa UNICEF

UNICEF inakadiria kuwa itahitaji dola za Marekani milioni 3.5 ili kukabiliana na mahitaji ya haraka ya watu walioathiriwa na Kimbunga Ana na tayari imeanza kutumia vifaa vyake vilivyonunuliwa awali huku ikiendelea na uchangishaji fedha kwa wadau wa ndani.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Msumbiji Maria Luisa Fornara amesema wanafanya kazi pamoja na serikali ya Msumbiji na washirika wengine kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watoto na familia zao katika maeneo yaliyoathirika. “Kimbunga hichi likichoikumba Msumbiji ni ukumbusho wa wazi kwamba athari za mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri na watoto wanaathiriwa zaidi na hali mbaya ya hali ya hewa inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.” 

Timu za dharura za UNICEF katika siku chache zijazo zitaanza kusambaza vifaa muhimu kama vile ndoo, sabuni na vidonge vya kusafisha maji, chakula cha matibabu kilicho tayari kutumika kwa watoto wenye utapiamlo, na wataweka maeneo maalum ya kujifunzia ambapo watoto ambao shule zao zimeharibika wanaweza kujifunza na kucheza kwa usalama. 

Kwakupitia simu za mkononi  na redio za mikoa na za jamii, UNICEF inashiriki katika kutoa jumbe za kuelimisha kujilinda na kujikinga ili wananchi waweze kupunguza athari za kimbunga hicho. 

Kwakuzingatia kuwa nchi ya Msumbiji ipo katika msimu wa mvua hivyo athari hizi za kimbunga zinaweza kuongezeka muda wowote kwakuwa vitu kama mito na mabwawa yamejaa maji ilihali mvua inaendelea kunyesha. 

Zaidi ya watu elfu 58.8 wameathirika na mvua kubwa na mafuriko Msumbiji tangu Desemba mwaka jana (Kutoka Maktaba)
UN Mozambique
Zaidi ya watu elfu 58.8 wameathirika na mvua kubwa na mafuriko Msumbiji tangu Desemba mwaka jana (Kutoka Maktaba)

Msumbiji na majanga ya vimbunga 

Kuanzia 2016 hadi 2021, Msumbiji imekabiliwa na matukio mawili ya ukame na vimbunga ikiwa ni pamoja na Cyclones Idai na Kenneth ambayo ilipiga nchi hiyo mwaka 2019 na ndani ya muda wa wiki sita na kuathiri watu milioni 2.5. 

Kulingana na chombo cha kutathmini hatari ya maafa INFORM, Msumbiji inashika nafasi ya 9 kati ya nchi 191 duniani kutokana na hatari kubwa ya nchi hiyo kukumbwa na hatari, kukabiliwa na hatari, na ukosefu wa uwezo wa kukabiliana nayo.