Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto bilioni 1 wako hatarini kutokana na janga la tabianchi: UNICEF na wadau

Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Horseed ambayo ni moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na ukame Somalia
WFP/Geneva Costopulos
Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Horseed ambayo ni moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na ukame Somalia

Zaidi ya watoto bilioni 1 wako hatarini kutokana na janga la tabianchi: UNICEF na wadau

Tabianchi na mazingira

Zaidi ya watoto bilioni moja wako katika hatari kubwa ya athari za janga la tabianchi, kwa mujibu wa ripoti mpya kuhusu Hatari za Tabianchi kwa Watoto iliyofanywa na Muungano wa Mpango wa Haki za Mazingira za Watoto (CERI) ambao unahisisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF, Plan International na Save the Children. 

Watoto wanaangushwa na ahadi za ufadhili kwa tabianchi, licha ya kubeba mzigo mkubwa wa janga la tabianchi, yamesema mashirika hayo. 

Taarifa iliyotolewa leo Juni 22 mjini Paris, Ufaransa imesema kuna ushahidi kwamba mabadiliko ya tabianchi yanatatiza watoto kupata huduma za msingi kama vile elimu, huduma za afya na maji safi ya kunywa. 

UNICEF na washirika wake wameonesha kuwa ni asilimia 2.4 tu ya fedha za tabianchi duniani zinazofuata miongozo inayolenga idadi ya watoto. 

Sehemu hii inawakilisha dola za kimarekani bilioni 1.2 tu katika uwekezaji katika kipindi cha miaka 17 na kwamba zaidi ya watoto bilioni moja wana uwezekano mkubwa wa kuteseka kutokana na athari za janga la tabianchi. 

Utafiti unazingatia vigezo vitatu vya kutathmini utoshelevu wa mahitaji ya watoto. Unazingatia hatari mahususi na zinazokithiri ambazo wanakabiliana nazo, unaimarisha uthabiti wa huduma za kijamii kwa kundi hili, na kuwawezesha watoto kama mawakala wa mabadiliko. 

Ufadhili wa "kushughulikia dhuluma" 

UNICEF ​​pia inasema mabadiliko ya tabianchi yanadhoofisha upatikanaji wa huduma za msingi kwa watoto kama vile elimu, huduma za afya na maji safi. 

Kulingana na mkuu wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa Shirika la Save the Children, Kelley Toole, watoto, hasa wale ambao tayari wameathiriwa na ukosefu wa usawa na ubaguzi, "wamechangia kidogo mno katika kusababisha mabadiliko ya tabianchi, lakini wanaathiriwa zaidi na hali hiyo." 

Kwake, fedha za tabianchi "zinatoa fursa ya kushughulikia dhuluma hizi, kwa kuzingatia mahitaji na mitazamo ya watoto."