Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila sekunde 39 mtoto 1 hupoteza maisha kutokana na kichomi:UNICEF 

Watoto wakipatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu katika wilaya ya Dondo nchini Msumbiji.
UN
Watoto wakipatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu katika wilaya ya Dondo nchini Msumbiji.

Kila sekunde 39 mtoto 1 hupoteza maisha kutokana na kichomi:UNICEF 

Afya

Ugonjwa unaozuilika wa kichomi unakatili maisha ya watoto  wengi kuliko maradhi mengine yoyote kwa mujibu wa taarifa ya utafiti mpya iliyotolewa leo na mashirika matano ya kimataifa yanayohusika na masuala ya watoto likiwemo la Umoja wa Mataifa la UNICEF. 

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na UNICEF, ubia wa chanjo duniani GAVI, Save the children, Every Breath Counts na Unitaid,  kwa mwaka jana pekee ugonjwa wa kichomi ulikatili maisha ya watoto zaidi ya laki 8 walio na umri wa chini ya miaka mitano sawa na mtoto 1 kila sekunde 39.

Utafiti huo umesema vifo vingi hutokea kwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili na takribani vifoo 153,000 hutokea ndani ya mwezi mmoja wa maisha yao.

Ili kutoa tahadhari ya ugonjwa huo uliosahaulika mashirika hayo matano leo yamezindua wito wa kimataifa wa kuchukua hatua ambao utafuatiwa na kongamano la kimataifa la ugonjwa wa kichomi utotoni litakalofanyika nchini Hispania mwezi Januari mwakani.

Akisisitiza kuhusu ukubwa wa tatizo hilo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema “Kila siku karibu watoto 2,200 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki duniani kutokana na kichomi ugonjwa unaotibika na kuzuilika, hivyo hatua imara za kimataifa na kuongeza uwekezaji ni muhimu kukabiliana na ugonjwa huu. Ni kwa kupitia miradi ya gharama nafuu, kinga na matibabu kufikishwa waliko watoto walioathirika ndipo tutaweza kuokoa maisha ya mamilioni ‘’

Kichomi ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria , virusi au fangasi na hufanya watoto kupata matatizo ya kupumua kutokana na mapafu yao kujaa usaha na maji.

Kwa mwaka 2018 utafiti huo unasema watoto wengi zaidi wa chini ya umri wa miaka 5 walikufa kwa  kichomi kuliko ugonjwa mwingine wowote, mwaka ambao ulishuhudia vifo vya watoto kutokana na ugonjwa kwa kuhara   437,000 walio chini ya umri wa miaka 5 na vifo 272,000 vilivotokana na malaria kwa watoto wa umri huohuo.

Na nchi tano ndizo zilizohusika na idadi zaidi ya nusu ya vifo vyote vya kichomi duniani kwa mwaka jana ambazo ni Nigeria (162,000), India (127,000), Pakistan (58,000) Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC (40,000) na Ethiopia (32,000). Nchi nyingine zilizoathirika na ugonjwa huu ni Indonesia (19,000), China (18,000) , Chad (18,000), Angola( 16,000) na Tanzania (15,000)

Hali halisi ya ugonjwa huu

UNICEF na wadau wanasema ugonjwa huo unaweza kuzuiliwa kwa chanjo na kutibika kirahisi kwa dawa za gharama nafuu za viuavijasumu endapo watafanyiwa vipimo kwa umakini. Lakini mamilioni ya watoto hawapati chanjo na mtoto mjoja kati ya watutu wenye dalili za ugonjwa huo hawapati huduma muhimu za afya zinazostahili.

Kwa mujibu wa uatafiti huo watoto walioathirika vibaya na kichomi wanaweza kuhitaji matibabu ya hewa ya oxijeni ambayo si rahisi kupatikana katika nchi masikini ambako watoto huhitaji huduma hiyo.

Kwa upande wake mwenyekiti mtendaji wa muungano wa chanjo duniani GAVI , Dkt. Seth Berkley amesema “ukweli kwamba ugonjwa huu ambao unazuilika, unatibika na kupinmwa kirahisi kuendelea kuwa ugonjwa unaouwa Watoto Zaidi ya maradhi mengine inashangaza. Tumepiga hatua kubwa katika muongo mmoja uliopita , na mamilioni ya watoto katika nchi masikini hivi sasa wanapata chanjo ya kichoni, lakini bado tuna kibarua kigumu cha kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata fursa ya chanjo hiyo ya kuokoa maisha.”

Wito wa mashirika hayo kwa dunia

Kwa pamoja mashirika hayo UNICEF, GAVI, Save the children, Every Breath Counts na Unitaid yamesema kwa miongo sasa muuaji mkubwa wa Watoto amekuwa ni ugonjwa uliopuuzwa na Watoto hao wasiojiweza kote duniani wamekuwa wakilipa gharama kubwa. “Sasa umewadia wakati kwa serikali, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa, makampuni, na mashirika yasiyo ya kiserikali kujiunga pamoja kupambana na kichoni na kuwalinda watoto hawa.”

Mashirika hayo yamezitaka serikali katika maeneo yaliyoathirika zaidi kuunda na kutekeleza mkakati wa kudhibiti kichomi na kupunguza vifoo vya watoto vitokanavyo na ugonjwa huo kwa kuboresha huduma za afya za msingi kama sehemu ya huduma za afya kwa wote.

Pia wamezitaka nchi Tajiri, wahisani wa kimataifa na nmakampuni ya sekta binafsi kupiga jeki masuala ya chanjo kwa kupunguza gharama ya chanjo za muhimu na kuhakikisha mafanikio ya GAVI na pia kuongeza ufadhili kwa ajili ya masuala ya utafiti na ubunifu wa kupambana na kichomi.