Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Filippo Grandi azuru Kenya kukutana na wakimbizi na viongozi wa kitaifa

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi akikutana na mkimbizi wa Somalia Abdulaziz Lugazo, katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.
© UNHCR/Samuel Otieno
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi akikutana na mkimbizi wa Somalia Abdulaziz Lugazo, katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.

Filippo Grandi azuru Kenya kukutana na wakimbizi na viongozi wa kitaifa

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi, (UNHCR) Filippo Grandi yuko nchini Kenya kwa ziara ya siku nne ambayo pia ameitumia kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani.  


 

Jana Jumatatu ametembelea makazi ya wakimbizi ya Kalobeyei huko Kakuma, kaskazini-magharibi mwa Kenya, ambapo ametangamana na wakimbizi na jamii ya eneo hilo na kushiriki katika hafla za kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 20.  

Kaulimbiu ya Siku ya Wakimbizi Duniani ya mwaka huu 2023 ni ‘Matumaini mbali na nyumbani – ulimwengu ambapo wakimbizi wanajumuishwa kila mara.’ 

Grandi amesema anashukuru sana kuwa nchini Kenya, ambayo inachukua mbinu bunifu kuwapa wakimbizi matumaini zaidi - na fursa zaidi - wanapokuwa mbali na nyumbani. 

Mtazamo wa Grandi unahimiza nchi nyingi zaidi ulimwenguni kuiga mfano huo. 

Kenya, ambayo imehifadhi wakimbizi kwa zaidi ya miaka 30, inatazamiwa kuzindua sera bunifu na jumuishi kuruhusu baadhi ya wakimbizi na waomba hifadhi nusu milioni inayowahifadhi kufanya kazi na kuishi na Wakenya. 

Hii itafungua njia ya kujitegemea, kukuza uchumi wa ndani, na kupunguza utegemezi wa misaada ya kibinadamu. 

Grandi amesema anaitumia ziara hii kuangazia ulimwengu mzima kwamba mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kutoa matumaini kama hayo, fursa na suluhisho kwa wakimbizi, popote walipo na kwa muktadha wowote. 

Mkuu huyo wa UNHCR, katika ziara ya siku 4 nchini humo, atafanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Serikali ya Kenya kuhusu mbinu mpya ya usimamizi wa wakimbizi nchini Kenya.