Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je tutaungana pamoja au tutawapa visogo wakimbizi kutatua madhila yao? -UNHCR

Kambi ya Kutupalong-Balukhali eneo la Cox's Bazar nchin Bangladesh ni makazi ya zaidi ya wakimbizi 600,000 wa kirohingya ambao hawana utaifa.
© UNICEF/Bashir Sujan
Kambi ya Kutupalong-Balukhali eneo la Cox's Bazar nchin Bangladesh ni makazi ya zaidi ya wakimbizi 600,000 wa kirohingya ambao hawana utaifa.

Je tutaungana pamoja au tutawapa visogo wakimbizi kutatua madhila yao? -UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Suala la ulinzi wa wakimbizi ni moja ya vipaumbele vya awali kabisa vya Umoja wa Mataifa takriban miongo saba iliyopita hata hivyo, ufurushwaji wa watu bado unazua wasiwasi mkubwa kimataifa. Taarifa kamili na Arnold Kayanda

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi katika mkutano wa 70 wa programu wa kamisheni kuu ya shirika hilo uliofanyika mjini Geneva, Uswisi, mkutano ambao una lengo la kuchagiza nchi kusaidia mamilioni ya watu kote ulimwenguni wanaoishi bila utaifa amesema hatua zaidi zinahitajika, miaka tano tangu kuzinduliwa kampeni ya #IBelong ya kumaliza ukosefu wau taifa.

Bwana Grandi amesema, miongo saba baada ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa licha ya mazingira tofauti lakini utata wa suala la wakimbizi bado unasalia, akisema kwamba janga la zama za sasa la wakimbizi ni sehemu ya uhamiaji wa binadamu unaochochewa na mambo mbali mbali, ikiwemo mizozo kwa sababu ya raslimali ambayo inavuka mipaka kufuatia maslahi ya kikanda na kimataifa inayochangiwa pia na misimamo mikali, magenge ya wahalifu na ya mjini, ukosefu wa matumaini wakati dunia ikishuhudia maendeleo ya kielimu, na vita dhidi ya njaa na magonjwa vikikosa kuwafikia walio na mahitaji zaidi.

Maamuzi magumu yanayokumba wakimbizi

Aidha aina hatarishi za utaifa na hotuba za chuki ambazo huenezwa mitandaoni wakati mazingira hayo yakisababisha uwepo wa wakimbizi kutokana na hitilafu hizo. Na  hii ikiwa ni ishara ya mambo kwenda mrama. Kamishna Mkuu huyo amehoji,“ni nini tutafanya katika muongo mmoja ujao, je tutarudi nyuma na kusahau tuliyojifunza katika karne ya ishirini au tutashikamana licha ya tofuati zetu na kuchukua changamoto na fursa za ushirikiano wa kimatifa na kutatua madhila ya wakimbizi? Natoa wito kwenu nyote kuhakikisha uwakilishi wa mataifa, kubadilishana uzoefu chanya na kuweka ahadi zenye matokeo ambazo zitaimarisha mustakabali wa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.”

Mifumo hatarishi ya utaifa inatishia juhudi za kukabiliana na ukosefu wa utaifa

Bwana Grandi ameongeza kwamba hotuba za chuki na utafa usio na mwelekeo vinatishia juhudi za kukabiliana na ukosefu wa utaifa, licha ya uelewa wa umma kuhusu changamoto hiyo akisema kuwa, “mafanikio bado hayatabiriki; mifumo ya utaifa na tamko dhidi ya wakimbizi na waamiaji ni mienendo ambayo inahatarisha kugeuza hatua kurudi nyuma.”

Licha ya hali hiyo lakini kuna baadhi ya nchi ambazo zimejizatiti katika kukabiliana na suala la wakimbizi ambako Grandi ametolea mfano baadhi ya nchi, “serikali Afrika Mashariki na pembe ya Afrika wamekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mfumo jumuishi kwa wakimbizi ambapo Ethiopia, Djibouti, Kenya na Uganda miongoni mwa nchi zingine wamepiga hatua kubwa kwa msaada wa Benki ya dunia na uwekezaji wa sekta binafsi.” 

Ameongeza kwamba, “hii tayari inabadilisha maisha ya wakimbizi wengi pamoja na jamii zinazowahifadhi katika ukanda mzima.”  

Kwa upande wake balozi mwema wa UNHCR, Cate Blanchett amehimiza mataifa kwenye mkutano kufanya mengo zaidi kusaidia kukabiliana na madhila ya wasio na utaifa. Akitaja madhila yanayowakabili watu wasio na utaifa mcheza filamu huyo kutoka Australia amesema kwamba wasio na utaifa wananyimwa fursa ya kupata huduma ambazo walio na utaifa huenda wakazichukulia kama za kawaida kwa mfano, elimu, huduma ya afya, usafiri au hata kufungua akaunti ya benki.

Cate Blanchett, ambaye ni balozi mwema wa UNHCR akizungumza na wanahabari mjini Geneva, Uswisi
UN News/Daniel Johnson
Cate Blanchett, ambaye ni balozi mwema wa UNHCR akizungumza na wanahabari mjini Geneva, Uswisi

Bi Blanchet ametolea mfano suala la wakimbizi warohingya waliosaka hifadhi nchini Bangladesha amesema, “Kiwango cha shida kinachosababishwa na ukosefu wau taifa wa warohingya ni kubwa, na kile ambacho huanzia mashinani huenda kikaendelea kwa muongo mmoja hadi mwingine na inakuwa changamoto zadi ya mipaka ya nchi na kuwa janga la kimatifa. Kwa hiyo hebu tusikubali maswala mengine ya ukosefu wau taifa yakafikia viwango vya Rohingya.”

Hadi sasa ni nchi takriban 200 ambazo zimeahidi kufanya kazi na UNHCR kuhusu suluhu za ukosefu wa utaifa, ambao UNHCR inatarajia kutokomeza ifikapo mwaka 2024.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina J. Mohammed akizungumza katika mkutano huo amesema kukabiliana na suala la ufurushwaji na ukosefu wa utaifa una uhusiano na ajenda ya mwaka 2030 ya malengo endelevu kuhakikisha waliotengwa wanachangia na kujumishwa katika maswala ya kijamii na maendeleo ya kiuchumi, na kwamba“namna tutavyokabiliana na suala la wakimbizi katika muongo ujao itakuwa ni moja ya vipimo kuhusu mafanikio na ujumuishwaji, mkutano wa Desemba kuhusu wakimbizi kimatifa utakuwa ni fursa nzuri ya kutekeleza mkataba wa wakimbizi na kutekeleza azma ya kutomuacha mtu yeyote nyuma.”