Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 100 wamelazimika kufungasha virago na kuwa wakimbizi:UN

Watoto wakimbizi wa Sudan Kusini wakitembea pamoja baada ya kutoka shuleni kwenye makambi ya wakimbizi ya Nyumanzi Uganda
© UNICEF/Jiro Ose
Watoto wakimbizi wa Sudan Kusini wakitembea pamoja baada ya kutoka shuleni kwenye makambi ya wakimbizi ya Nyumanzi Uganda

Zaidi ya watu milioni 100 wamelazimika kufungasha virago na kuwa wakimbizi:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika siku ya wakimbizi duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakimbizi wanawakilisha roho bora zaidi ya kibinadamu.

Wanahitaji na wanastahili kuungwa mkono na mshikamano  sio mipaka iliyofungwa na kurudi nyuma walikotoka.

Katika ujumbe wake maalum wa kuadhimisha siku hii Katibu Mkuu amesema  tunakabiliana na takwimu za kushangaza kwani “Zaidi ya watu milioni 100 wanaoishi katika nchi zinazokumbwa na mizozo, mateso, njaa na machafuko ya mabadiliko ya tabianchi wamelazimika kuyahama makazi yao. Hizi sio iadi kwenye kwenye ukurasa pekee, hawa ni wanawake, watoto na wanaume wanaofanya safari ngumu na mara nyingi wanakabiliwa na unyanyasaji, unyonyaji, ubaguzi na ukatili”.

Ameendelea kusema kwamba siku hii “inatukumbusha wajibu wetu wa kulinda na kusaidia wakimbizi na wajibu wetu wa kufungua njia zaidi zamsaada. Hii ni pamoja na suluhu za kuwapa wakimbizi makazi mapya na kuwasaidia kujenga upya maisha yao kwa utu.”

Makumi ya maelfu ya wakimbizi wamewasili Chad kutoka Sudan.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Makumi ya maelfu ya wakimbizi wamewasili Chad kutoka Sudan.

Nchi zinazohifadhi wakimbizi zisaidiwe

Bwana Guterres amesisitiza kwamba “Tunahitaji msaada mkubwa zaidi wa kimataifa kwa nchi zinazowakaribisha wakimbizi kama inavyotakiwa na mkataba wa kimataifa wa wakimbizi, ili kuongeza fursa za ufikiaji wa elimu bora, kazi zenye staha, huduma za afya, makazi na ulinzi wa kijamii.”

Akaenda mbali zaidi na kusema “Na tunahitaji ari ya kisiasa yenye nguvu zaidi ili kuleta amani, ili wakimbizi waweze kurejea salama makwao.”

Kauli mbiu ya siku ya wakimbizi duniani mwaka huu ni "Matumaini bali na nyumbani."

Guterres amehitimisha ujumbe wake kwa kutoa wito wito kwa ulimwengu kuunganisha matumaini ambayo wakimbizi wanayabeba mioyoni mwao.

“Hebu tulinganishe ujasiri wao na fursa wanazohitaji, katika kila hatua yao”.