Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 100 kote duniani wamelazimika kufungasha virago na kukimbia makazi yao:UNHCR ripoti 

UNHCR imewapatia wakimbizi wa Burundi ardhi nchini DRC kwa ajili ya kilimo.
© UNHCR/Antonia Vadala
UNHCR imewapatia wakimbizi wa Burundi ardhi nchini DRC kwa ajili ya kilimo.

Zaidi ya watu milioni 100 kote duniani wamelazimika kufungasha virago na kukimbia makazi yao:UNHCR ripoti 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, lilisema kutokuwa na uhakika wa chakula duniani kote, janga la mabadiliko ya tabianchi, vita nchini Ukraine na dharura nyinginezo kuanzia Afrika hadi Afghanistan ndio sababu kubwa zilizowafanya watu milioni 100 kufungasha virago na kukimbia makwao.

Kupitia ripoti ya shirika hilo iliyotolewa leo kamishina mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema "Kila mwaka katika muongo uliopita, idadi ya wanaolazimika kukimbia makwao imekuwa ikiongezeka. Ama jumuiya ya kimataifa italazimika kushikamana ili kuchukua hatua kushughulikia janga hili la kibinadamu, kutatua migogoro na kusaka suluhu za kudumu, la sivyo hali hii mbaya itaendelea." 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kila mwaka ya mwelekeo wa kimataifa wa watu wanaotawanywa “Leo hii mtu 1 kati ya kila watu 78 duniani amehama, ni mabadiliko makubwa ambayo ni wachache wangeyatarajia muongo mmoja uliopita.” 

Kufikia mwisho wa 2021, idadi ya waliokimbia makazi yao kutokana na vita, ghasia, mateso na ukiukwaji wa haki za binadamu ilifikia watu milioni 89.3, kulingana na ripoti hiyo. 

“Hiyo ilikuwa ni ongezeko la asilimia nane kutoka mwaka 2020 na ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya miaka 10 iliyopita", wamesema waandishi wa ripoti hiyo wakihusisha ongezeko la mwaka jana na migogoro mingi inayoongezeka na mipya iliyozuka. 

Kichocheo cha uhaba wa chakula 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNHCR idadi ya watu milioni 100 waliokimbia makazi yao ilifikiwa mwezi Mei mwaka huu, wiki 10 tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kusababisha uhaba mkubwa wa nafaka na mbolea duniani kutoka kwa wauzaji hao wakubwa wa bidhaa nje hali ambayo wahudumu wa kibinadamu wa  wafadhili wa Umoja wa Mataifa wameipokea kwa hofu kubwa. 

Alipoulizwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva kama mgogoro wa kutokuwa na uhakika wa chakula duniani unaoendelea hivi sasa unaweza kusukuma watu wengi zaidi kukimbia makwao, kamishna mkuu Grandi amesema "hawezi kufikiria ni kwa jinsi gani inaweza kuwa vinginevyo.” 

Ameongeza kuwa "Endapo unakuwa na mgogoro wa chakula kuongezea na changamoto zingine za vita, ukiukwaji wa haki za binadamu, mabadiliko ya tabianchi, vitaongeza tu mwelekeo ulioelezewa katika ripoti hii na ambao tumeshuhudia ukiongezeka tayari katika miezi michache ya kwanza ya mwaka huu.” 

Ameongeza kuwa hii ilimaanisha kwamba kile ambacho nchi zilikuwa zikifanya kuhimili kupanda kwa bei ya nafaka na mafuta kilikuwa na umuhimu mkubwa pia kuzuia idadi kubwa ya watu kuhama makwao, "ambapo ukiniuliza wangapi, sijui, lakini inaweza kuwa idadi ni kubwa sana." 

Familia kutoka Eritrea ikiwa kwenye kituo cha muda Romani wakisubiriwa kuhamishwa hadi Netherlands.
© UNHCR/Stefan Lorint
Familia kutoka Eritrea ikiwa kwenye kituo cha muda Romani wakisubiriwa kuhamishwa hadi Netherlands.

Kuhama kunakochangiwa na migogoro 

Ripoti inasema kwa ujumla, nchi 23 zenye jumla ya watu milioni 850 zinakabiliwa na migogoro ya wastani au ya kiwango cha juu, ikitoa takwimu kutoka kwa  Benki ya Dunia. 

Imeendelea kusema miongoni mwa watu milioni 89.3 waliokimbia makazi yao mwaka jana, milioni 27.1 walikuwa wakimbizi , milioni 21.3 chini ya mamlaka ya UNHCR, na Wapalestina milioni 5.8 chini ya uangalizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA. 

Watu wengine milioni 53.2 walikuwa wakimbizi wa ndani, milioni 4.6 walikuwa wanaotafuta hifadhi na milioni 4.4 walikuwa raia wa Venezuela walioachwa bila chaguo ila kukimbia mzozo wa kiuchumi na kisiasa wa nchi yao. 

Takwimu kutoka kwa ripoti hiyo ya UNHCR zinasisitiza jukumu muhimu lililofanywa na mataifa yanayoendelea duniani katika kuwapa hifadhi watu waliokimbia makazi yao, huku mataifa yenye kipato cha chini na cha kati yakihifadhi zaidi ya wakimbizi 4 kati ya 5 duniani. 

Ikiwa na wakimbizi milioni 3.8 ndani ya mipaka yake, Türkiye inahifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, ikifuatiwa na Colombia, yenye wakimbizi milioni 1.8 (ikiwa ni pamoja na raia wa Venezuela), Uganda na Pakistan zinahifadhi wakimbizi milioni 1.5 kila moja na Ujerumani ikihifadhi wakimbizi milioni 1.3. 

Ikilinganishwa na idadi ya watu kitaifa, kisiwa cha Caribbea cha Aruba kilikuwa na idadi kubwa zaidi ya Wavenezuela waliokimbilia nje ya nchi 1 kati ya 6, wakati Lebanon ilikuwa mwenyeji wa idadi kubwa zaidi ya wakimbizi 1 kati ya 4, ikifuatiwa na Curacao 1 kati ya 10, Jordan 1 kati ya 14 na Türkiye 1 kati ya 23. 

Zahma kwa mamilioni 

Miongoni mwa majanga mapya makubwa ya kibinadamu yaliyoangaziwa mwaka 2021, UNHCR ilibainisha kuwa vita katika eneo la Tigray nchini Ethiopia ilisukuma takriban watu milioni 2.5 zaidi kuyahama makazi yao ndani ya nchi yao, huku wengine milioni 1.5 kati yao wakirejea makwao mwaka huo. 

Huko Afghanistan ripoti inasema uchukuaji madaraka wa Taliban mjini Kabul mwezi Agosti 2021 ulisababisha idadi kubwa ya watu kuwa wakimbizi wa ndani na wengine kukimbia katika mataifa jirani.  

Idadi ya watu waliokimbia makazi yao iliongezeka kwa mwaka wa 15 mfululizo, limesema shirika la UNHCR hatahivyo ripoti hiyo imesema  zaidi ya Waafghanistan 790,000 walirejea makwao mwaka huo. 

Hatimaye, nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, Nigeria, Sudan Kusini, Sudan, Syria na Yemen ripoti imesema zilishuhudia ongezeko la kati ya watu 100,000 na 500,000 waliolazimika kukimbia makazi yao mwaka 2021.