Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujenga miji inayojali wanawake tunahitaji kuwajenga wanawake kama miji: UN-HABITAT

Rachel Ruto, mke wa Rais William Ruto wa Kenya akizungumza katika hafla ya wanawake na wake wengine wa marais katika Mkutano wa UN-HABITAT, Nairobi Kenya.
© IISD/ENB Mike Muzurakis
Rachel Ruto, mke wa Rais William Ruto wa Kenya akizungumza katika hafla ya wanawake na wake wengine wa marais katika Mkutano wa UN-HABITAT, Nairobi Kenya.

Kujenga miji inayojali wanawake tunahitaji kuwajenga wanawake kama miji: UN-HABITAT

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Siku ya pili ya mkutano wa pili wa Baraza la shirika la Umoja wa Mataifa la  Makazi  duniani UNHABITAT hapo jana ilifunguliwa kwa mkutano wa kwanza kabisa kati ya mke wa Rais wa Kenya, Mheshimiwa Mama Rachel Ruto, na mkurugenzi mtendaji wa UN-Habitat, Maimunah Mohd Sharif, wakijadili kuhusu jukumu muhimu wa wanawake katika kuunda miji endelevu, salama, na yenye mnepo.

Mkutano huo uliopewa jina "Wanawake na jukumu lao katika kuunda miji na jamii." uliandaliwa na mke wa Rais wa Kenya.

Lengo la majadiliano lilikuwa kutambua jukumu muhimu la wanawake katika kuwezesha miji na jamii kustawi.

Mke wa Rais wa Uturuki, Bi. Emine Erdogan, alituma ujumbe wa video katika majadiliano hayo.

Mke wa Rais wa Botswana, Neo Masisi, pia alituma ujumbe wa video unaoonyesha kazi yake kuhusu uwezeshaji wa wanawake.

Majadiliano hayo yaliongozwa na mwanahabari maarufu wa Televisheni nchini Kenya Victoria Rubadiri.

Mke wa Rais Rachel Ruto(kushoto) akizungumza katika hafla ya wanawake mezani na wake wengine wa Marais katika Bunge la HABITAT, Nairobi Kenya.
© IISD/ENB Mike Muzurakis
Mke wa Rais Rachel Ruto(kushoto) akizungumza katika hafla ya wanawake mezani na wake wengine wa Marais katika Bunge la HABITAT, Nairobi Kenya.

Wanawake ni kioo cha jamii

Mke wa Rais wa Kenya alieleza kwa ufasaha umuhimu wa kuelekeza mazungumzo haya kwa wanawake katika hotuba yake ya ufunguzi.

Amewaelezea wanawake kama "kioo cha jamii", akionyesha kwamba mwanamke "lazima awe mezani wakati wa kupanga miji yetu, kwa sababu wao ni chembechembe ya jamii".

Mama Rachel Ruto ameongeza kuwa "Tuna imani kwamba matokeo ya mazungumzo ya leo yatasaidia sana katika kuunga mkono na kufikia lengo la maendeleo  la SDG 11, ambalo inahusu miji na jumuiya endelevu, na kupitia lengo la SDG 5, ambalo ni la usawa wa kijinsia, tutakuza sauti ya wanawake wetu kwa kuwashirikisha katika harakati za kuwa na jamii jumuishi, salama, thabiti na endelevu.”

Kampeni ya mama anafanya vizuri

Chini ya kampeni ya Mama anafanya vizuri”, Mke wa Rais wa Kenya amezungumza kuhusu programu nyingi anazosimamia kuunda miji na jamii endelevu na pia kukuza usawa wa kijinsia.

Mpango wake wa kuendesha baiskeli, unaolenga kuwashirikisha waendesha baiskeli ili kukuza jamii zenye afya na uzingatiaji wa mazingira, ni mojawapo. Siku ilianza kwa usafiri wa baiskeli kutoka Ikulu kupitia eneo la katikati mwa jiji la Nairobi hadi jumba la ofisi za Umoja wa Mataifa huko Gigiri jijini Nairobi. Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Usalama Barabarani, Jean Tods, pia alihudhuria hafla hiyo ya baiskeli kuelezea uungaji mkono kwake wa usafiri mijini.

  Mama mmoja aendesha baiskeli akiwa amebeba mtoto mgongoni katika mkoa wa kusini Matebele, Zimbabwe.
UNICEF/Tsvangirayi Mukwazhi
Mama mmoja aendesha baiskeli akiwa amebeba mtoto mgongoni katika mkoa wa kusini Matebele, Zimbabwe.

Katika jumba la mkutano, wajumbe walisikia kutoka kwa Beatrice Achieng na Rose Njoki, ambao walinufaika na programu ya shirika la Joyful Women’s. Shirika hilo linawawezesha wanawake kutoka jamii zilizo hatarini kuokoa pesa, kuchukua mikopo na kuunda biashara kupitia benki za mezani.

UNHABITAT imepiga hatua kuwezesha wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat, Maimunah Mohd Sharif, ametanabaisha  hatua zilizopigwa na shirika hilo katika kuwawezesha wanawake duniani kote. Shukrani kwa kazi ya UN-Habitat nchini Afghanistan, wanawake wameweza kupata haki za ardhi na mali.

Katika mipango miji na muundo wa maeneo ya umma, mkakati wa nyenzo kwa ajili ya jiji la mwanamke ulizinduliwa ili kuwapa wanawake zana za kuhakikisha usawa wa kijinsia.

Ili kukuza uongozi wa wanawake katika siasa na utawala wa miji, mkuu huyo wa UN-HABITAT anaongoza mpango wa miji inayoongozwa na wanawake.

Mpango unaolenga kukuza uongozi wa wanawake na uwezeshaji wa kiuchumi kupitia ushirikiano na uwekezaji wenye tija.

"Lazima tuhakikishe kwamba ushiriki wa wanawake na wasichana katika kufanya maamuzi katika ngazi ya jamii," amesema Maimunah Sharif.

Umuhimu wa wanawake katika kusaka suluhu

Naye mke wa rais wa Uturuki, Bi. Emine Erdogan, ambaye ni bingwa wa harakati za kutokomeza taka na mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya kutokomeza taka, ameangazia umuhimu wa wanawake na washikadau katika kuunda suluhu.

"Ninaamini kwa moyo wote kwamba suluhu ambazo zitatoa mwanga kwa ubinadamu zitatekelezwa chini ya uongozi wa wanawake waanzilishi na wanaojitolea wote ambao ni rafiki wa mazingira waliokusanyika pamoja katika hafla ya mkutano huu."

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba “Wanawake kuwezeshwa kushiriki na kuongoza mazungumzo ya jinsi ya kuboresha miji na jamii zetu ni muhimu kwetu ili kufanya maendeleo. Hii haiwezi kufanyika bila kukabiliana na vikwazo vya utaratibu vilivyowekwa.”

Mkutano huo ulihitimishwa na kauli kutoka kwa Waziri wa mazingitra na utalii wa Botswana, Phildah Kereng, ambaye alisema Ili kujenga miji inayojali wanawake kwanza tunahitaji kuwajenga wanawake kama miji.”