Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miji endelevu ni muhimu katika kurejesha maisha bora baada ya COVID-19

Miji kama mji mkuu wa Korea Kusini Seoul ni watumiaji wakubwa wa nishati
Unsplash/Ethan Brooke
Miji kama mji mkuu wa Korea Kusini Seoul ni watumiaji wakubwa wa nishati

Miji endelevu ni muhimu katika kurejesha maisha bora baada ya COVID-19

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Miji itakuwa muhimu kwa ulimwengu kupata nafuu kutoka kwenye janga la COVID-19 na uchumi mbaya zaidi kwa miongo kadhaa, kwa mujibu wa ripoti mpya  iliyochapishwa hii leo na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na makazi, UN-Habitat. 

Ripoti ya Miji ya Dunia ya mwaka 2020, iliyotolewa leo Jumamosi siku ya miji duniani, inaonesha thamani ya ukuaji wa miji endelevu na jinsi inavyoweza kuchangia juhudi za ulimwengu za kujijenga upya kwa ubora baada ya janga.  

Mkurugenzi Mtendaji wa UN Habitat, Maimunah Mohd Sharif amesema, "ripoti ya Miji ya Ulimwengu ya mwaka 2020 inathibitisha kwa hakika kwamba miji na miji iliyopangwa vizuri, inayodhibitiwa, na inayofadhiliwa inaunda uchumi, kijamii, mazingira na thamani nyingine isiyojulikana ambayo inaweza kuboresha sana maisha ya wote.”

Miji inasababisha mabadiliko

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ulimwenguni, karibu asilimia 55 ya watu wote wanaishi katika maeneo ya mijini: takwimu ambayo inatarajiwa kuongezeka hadi karibu asilimia 70 ifikapo mwaka 2050. 

UN Habitat imesema miji imekuwa katika kitovu cha janga la COVID-19 na asilimia 95 ya maambukizi ya ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona, yanapatikana katika maeneo ya mijini. 

 

Thamani ya ukuaji wa miji 

UN-Habitat imeeleza kuwa miji inazalisha thamani ya kiuchumi wakati inapokuwa inafanya kazi vizuri kwa mfano kwa kutoa machaguo ya usafiri ambayo yanapunguza msongamano wa magari na kufupisha muda wa kusafiri na hivyo kuruhusu zaidi ajira zenye tija.  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe maalum wa siku hii ya miji amesema miji imebeba gharama kubwa ya janga la corona au COVID-19 lakini jamii katika miji hiyo zimedhihirisha thamani yake. 

Aidha ametaka jamii kuwekwa katika kiini cha miji ya baadaye akisema, "wakati jamii za mijini zinahusika katika sera na kufanya maamuzi, na kuwezeshwa na rasilimali fedha, matokeo yanajumuisha zaidi na kudumu.”