Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo cha maharage chamwondoa Sprina kwenye ‘utumwa’ wa tumbaku

Sprina Robi Chacha mkulima kutoka Kenya ameshinda tuzo ya mwaka huu ya siku ya kutovuta tumbaku duniani, inayoendeshwa na WHO kwa mchango wake wa sio tu kuacha kulima tumbaku na kugeukia maharage yenye madini ya chuma, bali pia kufundisha mamia ya wakuli…
WHO Africa Video
Sprina Robi Chacha mkulima kutoka Kenya ameshinda tuzo ya mwaka huu ya siku ya kutovuta tumbaku duniani, inayoendeshwa na WHO kwa mchango wake wa sio tu kuacha kulima tumbaku na kugeukia maharage yenye madini ya chuma, bali pia kufundisha mamia ya wakulima wenzake kulima maharage kwa ajili ya jamii yenye afya.

Kilimo cha maharage chamwondoa Sprina kwenye ‘utumwa’ wa tumbaku

Afya

Wahenga walinena mcheza kwao hutunzwa na ndivyo ilivyo hii leo kwa Sprina Robi Chacha, mkulima huyu nchini Kenya ambaye suluba na madhara ya kilimo cha tumbaku alichojifunza na kukitekeleza tangu akiwa mdogo, vilisababisha aachane na kilimo hicho na kujikita na kilimo cha maharage yenye madini ya chuma.

Tuzo hiyo imetolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, (WHO) kwa kutambua mchango wa Sprina wa sio tu katika kukata shauri kuachana na kilimo cha tumbaku bali pia kuchukua hatua ya kukuza jamii yenye afya kupitia mlo wa maharage ambayo yana protini.

Kilimo cha tumbaku ni suluba na hupumziki

Video ya WHO, Kanda ya Afrika, inaanza kwa kuonesha nyakati za asubuhi nchini Kenya, umande na ukungu ni dhahiri Sprina akitazama picha za wazazi wake huku taswira ya kwenda shambani enzi hizo na jembe begani zikimjia anasema,“kilimo cha tumbaku ni cha suluba na kinachosha. Ni kwamba huna muda wa kupumzika, kwa sababu unahitaji muda mrefu sana shambani; kukagua shamba, kupulizia dawa kwa sababu tumbaku si stahmilivu kwa magonjwa na wadudu waharibifu wa mimea. Hivyo tulipatiwa dawa nyingi za kudhibiti wadudu hao shambani.”

Dawa za kuulia wadudu zilikuwa na gharama kubwa

Kwa mujibu wa Sprina, kampuni za tumbaku ziliwapatia dawa hizo kwa njia ya mkopo, lakini kwa gharama kubwa sana na kwamba, “baadhi ya hizo dawa za kuua vijidudu zilikuwa ni kali mno na zilikuwa na sumu na zilibabisha magonjwa kama vile magonjwa ya Ngozi, halikadhalika matatizo ya macho. Jambo lingine, kwa sababu ya kemikali nyingi zilizokuwa zinatumika, rutuba ya udongo ilipungua,  Bila kujua tulikuwa tunaharibu udongo wetu. Wakati wa mchakato wa kukausha tumbaku, moshi ulikuwa na sumu sana kwa macho yetu . Tumbaku ilileta uharibifu mkubwa.”

Wazazi wangu hawakufahamu zao mbadala la biashara kwa tumbaku

Sasa Sprina anatazama picha za wazazi wake huku akikumbuka kuwa enzi hizo za kilimo, tumbaku ilikuwa ndio zao pekee la kibiashara la kuwezesha wazazi wao kupata kipato. Hivyo tatizo lilikuwa ukosefu wa taarifa kuhusu zao lingine la kibiashara badala ya tumbaku. Tumbaku ikishamiri, tatizo lingine likashamiri pia.

“Uzalishaji chakula ulikuwa kidogo sana. Kwa sababu mtu ulihitaji eneo kubwa la kulima tumbaku ili upate faida. Hivyo basi mazao mengine ya chakula yalipata eneo dogo mno ambalo halikutosha kuzalisha chakula cha kutosheleza familia.”

Kilimo cha tumbaku kinatumikisha watoto

Watoto nao kuna nyakati hawakwenda shule ili wasaidie kilimo cha tumbaku. Jambo ambalo Sprina anasema ilikuwa ni utumikishaji wa watoto. Sprina alijitafakari akaona faida ya tumbaku ni hasara zaidi kuliko kulima mazao ya chakula.

Ukombozi kutoka WHO wabisha hodi kwa Sprina

Ndipo maafisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO walifika kijijini na kuzungumza na kikundi chao.

 “Walifika wakazungumza na sisi, na walitupatia mbegu ili kutuhamasisha tuchukue hatua ya kulima maharage yenye madini ya chuma kama zao mbadala la tumbaku.”

Sprina anasema alikubali haraka na akachukua hatua ya kutorejea kwenye kilimo cha tumbaku kwa kuwa, “tukijaribu kulinganisha kilimo cha tumbaku na maharage, kuna tofauti. Maharage yenye madini  ya chuma yanastahimili magonjwa, ukame na pia hayaharibu udongo bali yanarutubisha kupitia Naitrojeni. Pia inatupatia fedha nyingi kwani ukivuna tu unauza.”

Zaidi ya  yote anasema, sasa anaweza kupata kipato kizuri katika muda mfupi. Pia ana muda wa kupumzika na kuandaa mlo kamili kwa familia yake kwa kutumia  maharage. Watoto wana afya njema na ninajivunia. Wana muda wa kusoma na hakuna tena utumikishwaji. Wako tayari kusoma.