Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yawasaidia wakulima wa tumbaku Kenya, kuhamia katika mazao mbadala

Shamba la mmea wa tumbaku nchini Kenya
© WHO
Shamba la mmea wa tumbaku nchini Kenya

FAO yawasaidia wakulima wa tumbaku Kenya, kuhamia katika mazao mbadala

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limeimarisha afya ya wakulima wa kaunti ya Migori. Hii ni baada ya kuzindua machi Mwaka huu mradi wa kilimo mbadala unaolenga kusitisha kile cha tumbaku. Kwa ushirikiano wa WHO na WFP, FAO inajivunia mafanikio kwani afya za wakulima wa Migori zimeimarika baada ya kuacha kilimo cha tumbaku na kukiongeza kipato chao.

Mradi huo unajikita kwenye kilimo cha maharagwe, choroko na mazao mengine yanayochukua muda mfupi kukomaa. FAO inawapa elimu ya kiufundi na vifaa.

Mazao ya maharagwe, mahindi na viazi tamu ni vyakula ambavyo vinachukua muda mfupi kukomaa shambani. Shirika la Afya Ulimwenguni WHO na lile la Umoja wa Mataifa la Chakula na kilimo FAO pamoja na mpango wa chakula WFP, mnamo mwezi Machi mwaka huu  yalizindua mradi wa mazao yaliyo na virutubishi mwilini ili kuwaondoa wakulima kwenye kilimo cha tumbaku. Husna Mubarak ni afisa katika shirika la FAO na anaelezea,"tunachokifanya zaidi ni kuwapa elimu ya kiufundi kuhusu njia endelevu za kupanda mazao ambayo yanachukua muda mfupi shambani kabla ya kukomaa.Tunawapa mbegu na pia kuwaelezea jinsi ya kulima mazao ambayo yanalinda mazingira kwa kuhifadhi rutba ya mchanga.Kadhalika wanaliongeza pato lao kwani wakisitisha kilimo cha tumbaku wanahitaji njia mbadala ya kukidhi mahitaji yao.”

Wakulima wauza tani 135 za maharagwe

Mradi huu wa kilimo mbadala uko katika kaunti ya Migori. Wakulima wanaoshiriki kwenye mradi tayari wameuza tani 135 za maharagwe kwa mpango wa chakula wa Umoja wa Mataifa,WFP. Mazao haya yanawapa kipato kizuri zaidi ikilinganishwa na tumbaku ambayo inahitaji vifaa, nguvu kazi nyingi na muda mrefu kukomaa shambani. Mradi huu umeimarisha afya ya wakulima ambao awali walitatizwa na madhara ya tumbaku. Margaret Nyamataga aliacha kilimo cha tumbaku baada ya kupata madhara ya macho na anaweka bayana kuwa, "Tumbaku iliniharibu macho.Sasa sioni vizuri. Kila wakati nafikicha macho na siwezi hata kusoma vitabu vizuri bila miwani. Tulikuwa tukikata majani mabichi na miti ya aina yoyote ile ambayo inapatikana huku kwetu kwa wingi.Ule moshi wake ndio uliokuwa unatuathiri pale tumbaku inafukizwa ili ikauke.”

Jones Rioba Mwita ni mkaazi wa Sakuri iliyoko Kuria mashariki na aliacha kilimo cha tumbaku na sasa anapanda vyakula vyenye manufaa mwilini. Kwa mtazamo wake ukosefu wa vifaa madhubuti ndio uliowaletea madhara kwenye kilimo cha tumbaku anasema, "nilitaka kuacha kilimo cha tumbaku kitambo lakini nilihitaji hela za kuwasomesha wanangu.Nilipoenda kwa daktari akaniambia nisipoacha basi sitaishi kwa muda mrefu.Nilikuwa mnene lakini sasa hali sio hiyo.Tulikuwa tukiwauliza, kwanini picha kwenye mifuko ya dawa na kemikali zinazotumika inaonyesha watumiaji wakivaa mabuti,barakoa na glavu na sisi hatuna? Naamini hilo ndilo lililotuletea madhara.”

Kenya na mkataba wa WHO

Ijapokuwa mradi huo unaendelea, bado wako wakulima wanaoamini mapato ya tumbaku ni mengi ikilinganishwa na madhara yake.

Kenya ni moja ya mataifa ya kwanza yaliyorasimisha mwaka 2004 mkataba wa shirika la afya ulimwenguni WHO unaodhibiti matumizi ya tumbaku. Serikali ya Kenya imekuwa mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya tumbaku na bidhaa zake ili kuilinda afya ya jamii. Jacob Gisiri ni mkulima na anaamini tumbaku iko sawa ukifuata kanuni zake, "tumbaku ina nicotine na ukiilima kisha utumie pombe au kuivuta utaangamia.Ukipanda tumbaku unatakiwa kuhakikisha unakula vizuri na kunywa maziwa kwa wingi ili uilinde afya yako.Walioacha kulima tumbaku ningewaambia wairejelee lakini kila mtu ana mipangilio yake maishani kwani kipenda roho nyama mbichi hula.Mimi napenda kilimo cha tumbaku kwani najisikia niko sawa.”

Awamu ya majaribio

Mradi huu wa kilimo mbadala unaolenga kusitisha kile cha tumbaku uko kwenye awamu ya majaribio kwenye eneo la Uriri la kaunti ya Migori. Mipango ipo kuwashirikisha wakulima wa eneo zima la Kuria Mashariki hadi mpakani na Tanzania.