Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni kubwa zaidi ya chanjo ya polio Afrika inayolenga watoto milioni 21 yaanza

Mtoto mvulana akipewa chanjo wakati wa kampeni ya chanjo ya polio huko Kisangani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Julai 2022.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Mtoto mvulana akipewa chanjo wakati wa kampeni ya chanjo ya polio huko Kisangani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Julai 2022.

Kampeni kubwa zaidi ya chanjo ya polio Afrika inayolenga watoto milioni 21 yaanza

Afya

Kampeni kubwa zaidi barani Afrika ya chanjo dhidi ya polio tangu 2020 inaanza leo katika nchi tatu za Afrika Magharibi na Kati, katika juhudi za pamoja za mamlaka ya kitaifa ya kutoa chanjo kwa watoto milioni 21 walio chini ya umri wa miaka mitano. 

Taarifa iliyotolewa nashirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani Kanda ya Afrika, WHO Afrika iliyotolewa hii leo mjini Brazzaville imeeleza zoezi hilo ambalo litaanza nchini Cameroon, Chad na Niger kabla ya kuongezwa hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati wiki ijayo, linakuja kudhibiti ugunduzi 19 wa virusi vya polio vya aina ya 2 katika nchi hizo; wagonjwa 2 nchini Niger, wagonjwa 10 nchini Chad, wagonjwa 4 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na wagonjwa 3 nchini Cameroon. 

Mkakati huo wa nchi nyingi unaungwa mkono na WHO kupitia Mpango wa Kutokomeza Polio Duniani (GPEI), na unajumuisha chanjo zilizounganishwa na pia mipango ya pamoja katika jumuiya za mpakani kukomesha maambukizi ya polio. 

"Hili ni jukumu muhimu la kuziba mapengo ya chanjo kutokana na janga la coronavirus">COVID-19 na litawapa mamilioni ya watoto ulinzi muhimu kutokana na hatari ya kupooza kwa ugonjwa wa kupooza," amesema Dkt Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika akiongeza kuwa "Kuunganisha kampeni hiyo kutahakikisha kuwa kundi kubwa la watoto katika nchi zote nne wanapokea chanjo hiyo kwa wakati mmoja ili kuimarisha kinga ya polio katika eneo pana la kijiografia." 

Eneo la bonde la Ziwa Chad linakabiliana na mojawapo ya matukio ya muda mrefu zaidi ya ghasia za kutumia silaha duniani. Pia ni nyumbani kwa idadi kubwa zaidi ya watoto wanaotambulika kwa mawasiliano ya chanjo kama "dozi sifuri" ulimwenguni, ambao hawajachanjwa au walichanjwa kidogo. 

Nchi zote nne zimefanya juhudi kubwa kuimarisha utambuzi wa polio, kuzuia kuenea kwa virusi na kuwalinda watoto dhidi ya hatari ya kuambukizwa na kupooza kwa maisha yote. Hata hivyo, licha ya kwamba wote wamethibitishwa kuwa hawana virusi vya polio mwitu lakini polio aina ya 2 inaendelea. 

Katika nchi zote, serikali zimeendelea kuboresha ubora wa shughuli za chanjo, zikiimarishwa na utekelezaji mpana wa kampeni za ziada za chanjo. Haya yanalengwa katika kushughulikia hatari zilizobaki za aina zote za virusi vya polio, huku pia zikiimarisha chanjo ya kawaida katika ngazi ya nchi. 

Aidha, usambazaji chanjo wa nyumba kwa nyumba umewapunguzia wazazi mzigo wa kuwasafirisha watoto wao katika vituo vya afya kupata chanjo. Wafanyakazi wa afya, kwa usaidizi kutoka kwa WHO, sasa pia wanatoa chanjo majumbani, na pia katika vituo vya kidini, sokoni na shuleni. 

Viongozi wa dini na jamii, kama mabingwa wa kutokomeza virusi vya polio, pia husaidia kuhamasisha walezi kuwachanja watoto wao sio tu dhidi ya polio, lakini magonjwa yote yanayoweza kuzuilika. 

Muhimu, data za kuaminika ni muhimu kwa ufuatiliaji wa magonjwa na hatua dhidi ya mlipuko. Kufuatia milipuko inayoendelea ya virusi vya polio vinavyozunguka, nchi pia zimeongeza ufuatiliaji ili kugundua visa.