Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika yahitaji kupatia chanjo watoto milioni 33 ili kurejea kwenye mwelekeo sahihi- WHO

Mtoto wa kiume mwenye umri wa chini ya miaka 5 akipatiwa chanjo dhidi ya Surua nchini Zimbabwe.
UNICEF
Mtoto wa kiume mwenye umri wa chini ya miaka 5 akipatiwa chanjo dhidi ya Surua nchini Zimbabwe.

Afrika yahitaji kupatia chanjo watoto milioni 33 ili kurejea kwenye mwelekeo sahihi- WHO

Afya

Takribani watoto milioni 33 barani Afrika watatakiwa kupatiwa chanjo kati ya mwaka huu wa 2023 na mwaka 2025 ili kurejesha bara hilo kwenye mwelekeo wa kufikia lengo la kimataifa la kupatia chanjo watoto ifikapo mwaka 2023.

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari huko Brazaville, Jamhuri ya Congo, wakati huu ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ripoti ikisema watoto milioni 67 walikosa chanjo moja au zote katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi sasa kutokana na COVID-19

Chanjo ambazo watoto wanatakiwa kupatiwa kati ya sasa na 2025 kwa mujibu wa WHO ni zile za kupunguza magonjwa na vifo , mathalani chanjo za kinga dhidi ya magonjwa. 

“Kila hatua inapaswa kuchukuliwa ili kila mtoto apate chanjo,” amesema Dkt. Moeti akiongeza bila utashi mpya wa kisiasa na juhudi kubwa zaidi za serikali, inakadiriwa kuwa utoaji wa chanjo kwa watoto Afrika hautarejea katika hali ya kawaida kabla ya COVID-19 hadi mwaka 2027.  

Ili kusaidia Afrika kuimarisha juhudi hizo, tayari WHO na wadau wanasaidia nchi 10 za Afrika ambazo ni miongoni mwa mataifa 20 duniani yenye idadi kubwa ya watoto wasio na chanjo ili kuhakikisha zinarejea kwenye mwelekeo sahihi wa utoaji chanjo. 

Wiki ya chanjo duniani inayoanza tarehe 24 hadi 30 mwezi huu wa Aprili itatumiwa kama mbinu ya wadau na nchi kuchagiza utoaji chanjo kupitia programu za chanjo.