Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 100 baada ya tetemeko Uturuki na Syria, mamilioni ya watoto na familia zao bado wanahaha: UNICEF

Watoto milioni mbili wanahitaji msaada nchini Uturuki.
© UNOCHA/Ahmad Abdulnafi
Watoto milioni mbili wanahitaji msaada nchini Uturuki.

Siku 100 baada ya tetemeko Uturuki na Syria, mamilioni ya watoto na familia zao bado wanahaha: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Siku mia moja baada ya kutokea kwa matetemeko mabaya zaidi ya ardhi katika historia ya hivi karibuni nchini Uturuki na Syria, mamilioni ya watoto na familia zao wanahaha kujenga upya maisha yao, huku watoto milioni 2.5 huko Uturuki na milioni 3.7 nchini Syria wakihitaji msaada wa kibinadamu unaoendelea limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika tarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Ankara, Damascus na Geneva Uswisi matetemeko hayo mawili ya awali yaliyosababisha uharibifu mkubwa tarehe 6 Februari 2023, yakifuatiwa na maelfu ya mitetemeko mingine midogo ya ardhi, yamesukuma familia nyingi ukingoni na kuwaacha watoto bila makazi na bila kupata huduma muhimu, ikiwa ni pamoja na maji salama, elimu na matibabu, na kuongezeka kwa hatari za ulinzi kwa watoto walio katika mazingira magumu.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell, ambaye alitembelea nchi zote mbili wiki chache baada ya matetemeko ya kwanza ya ardhi amesema "Baada ya matetemeko hayo ya ardhi, watoto katika nchi zote mbili wamepata hasara na huzuni isiyoelezeka. Matetemeko ya ardhi yalipiga maeneo ambayo familia nyingi tayari zilikuwa hatarini sana. Watoto wamepoteza familia na wapendwa wao, na kuona nyumba zao, shule na jamii zikiwa zimesambaratishwa na maisha yao yote yamepinduliwa.”

Umm Ahmad (sio jina lake halisi) alihamishwa na familia yake hadi kwenye kambi ya Al-Kamuna huko Sarmada, Idlib vijijini.
UN News / Shirin Yaseen
Umm Ahmad (sio jina lake halisi) alihamishwa na familia yake hadi kwenye kambi ya Al-Kamuna huko Sarmada, Idlib vijijini.

Hali ilikuwa mbayá hata kabla ya matetemeko

Kwa mujibu wa UNICEF hata kabla ya matetemeko ya ardhi ya hivi majuzi, familia nyingi katika maeneo yaliyoathiriwa zilikuwa zikihangaika.

“Katika mikoa ya Uturuki, viwango vya umaskini miongoni mwa watoto vilikuwa tayari viko juu na takriban asilimia 40 ya kaya zinaishi chini ya mstari wa umaskini, ikilinganishwa na karibu asilimia 32 inayoonekana kote nchini. Makadirio yanaonyesha kuwa bila msaada endelevu wa ndani na wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwapa fedha taslim na kuhakikisha upatikanaji wa elimu, takwimu hizi zinaweza kuongezeka hadi zaidi ya asilimia 50.”

Kwa sasa, watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika maeneo yaliyoathirika sana wanakabiliwa na vitisho ikiwa ni pamoja na ukatili, ndoa za shuruti au kazi ngumu, na kuacha shule.

“Elimu ya karibu watoto milioni nne walioandikishwa shule ilitatizika, wakiwemo zaidi ya watoto 350,000 wakimbizi na wahamiaji. Wakati Uturuki imepata maendeleo katika kupunguza hatari hizi katika miaka ya hivi karibuni, athari za matetemeko ya ardhi zinaweza kurudisha kazi hiyo iliyofanyika nyuma.”

Nchini Syria, watoto tayari walikuwa wakihangaika baada ya miaka 12 ya migogoro unaoendelea, ambaoo umekuwa na athari kwa miundombinu yote na huduma za umma limesema shirika la UNICEF.

“Matetemeko hayo makubwa ya mwezi Februari yalizidisha hali hii, na kusababisha uharibifu zaidi kwa shule, huduma za afya, na miundombinu mingine muhimu. Uharibifu mkubwa wa miundombinu ya maji na maji taka umewaweka watu milioni 6.5 katika hatari kubwa ya magonjwa ya maji, pamoja na kipindupindu.”

Wasichana wadogo wakicheza katika kituo cha mapokezi cha watu waliokimbia makazi yao huko Jindairis, mkoa wa Aleppo.
UN News/Shirin Yaseen
Wasichana wadogo wakicheza katika kituo cha mapokezi cha watu waliokimbia makazi yao huko Jindairis, mkoa wa Aleppo.

Watoto 51,000 hatarini kupata unyafuzi

“Takriban watoto 51,000 walio chini ya umri wa miaka mitano wana uwezekano wa kukumbwa na utapiamlo wa wastani na mkali au unyafuzi na wanawake 76,000 wajawazito na wanaonyonyesha wanahitaji matibabu kutokana na utapiamlo uliokithiri.” Limesema shirika hilo.

Watoto wengine wapatao milioni 1.9 wametatizika elimu yao, huku shule nyingi zikiendelea kutumika kama makazi.

Katika muda wote wa siku 100 zilizopita, wengi wao bado wanaishi katika hali ngumu sana, huku msongo wa mawazo ukizidishwa na kutokuwa na uhakika wa ziada wa kutojua ni lini wanahitaji kuhama kutoka nyumba moja hadi nyingine.

Bi. Russell amesema “Njia ya kupata nafuu ni ndefu, na familia zitahitaji msaada wetu unaoendelea. Athari za muda mrefu za maafa haya ni pamoja na kupanda kwa bei ya chakula na nishati pamoja na kupoteza maisha , uwezo wa kujikimu na upatikanaji wa huduma kutasukuma mamia kwa maelfu ya watoto katika umaskini zaidi.”

Amesisistiza kuwa “Endapo msaada wa kifedha na huduma muhimu hazitapewa kipaumbele kwa watoto hawa na familia kama sehemu ya mpango wa uokoaji wa haraka na wa muda mrefu, basi watoto wataendelea kuwa katika hatari kubwa ya kunyonywa na kunyanyaswa.”

Wito wa UNICEF kwa jumuiya ya kimataifa

UNICEF inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuweka kipaumbele katika juhudi za kujimwamua wa mapema zinazolenga mtoto na kuhakikisha kwamba mahitaji ya watoto yanatimizwa ndani ya mgao wa ufadhili.

Pia imesema uwekezaji lazima ufanywe katika juhudi za uokoaji, kwa msisitizo wa kurejesha mifumo bora, thabiti na inayojumuisha watu waliotengwa zaidi.

UNICEF imekuwa ikifanya kazi bila kuchoka tangu matetemeko ya ardhi kuongeza msaada wa haraka wa kuokoa maisha kwa jamii zilizoathiriwa, kutathmini athari za maafa na kusaidia ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na urejeshaji wa huduma za msingi.

Hata hivyo, msaada zaidi unahitajika ili kukabiliana na mzozo unaoendelea.

Vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na tetemeko kwenye moja ya mitaa ya kati ya jiji la Antakya, Hatay.
IOM 2023/Enver Mohammed
Vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na tetemeko kwenye moja ya mitaa ya kati ya jiji la Antakya, Hatay.

Uwekezaji zaidi ni muhimu

Ili kulinda haki za watoto na kuzuia kunyimwa zaidi kwa haki zao UNICEF inahimiza kuendelea kuwekeza katika maeneo muhimu, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kifedha kwa familia, upatikanaji wa elimu bora, na kupata msaada wa kisaikolojia na kijamii.

“Uwekezaji huu utasaidia kuondoa familia kutoka kwenye umaskini na kuzuia matokeo mabaya kama vile ndoa za utotoni na ajira ya watoto.” Limesema shirika la UNICEF

Kuendelea kufadhiliwa kwa programu za afya, lishe na maji, usafi wa mazingira na usafi ni muhimu katika kuhakikisha afya na ustawi wa watoto na kupunguza hatari za milipuko ya magonjwa.

Ili kukidhi mahitaji ya kuokoa maisha ya karibu watoto milioni 3 walioathiriwa na tetemeko la ardhi nchini Syria, UNICEF inaomba dola milioni 172.7 kutekeleza mpango wake wa kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi.

“Hadi sasa, dola milioni 78.1 zimepokelewa, huku lishe, afya na elimu zikisalia kuwa hazifadhiliwi kwa kiasi kikubwa.”

Nchini Uturuki, UNICEF bado inahitaji zaidi ya dola milioni 85 kati ya ombi la dola milioni 196 ili kutoa huduma zinazohitajika kwa watoto wenye uhitaji. Ingawa kuna mahitaji katika sekta zote, uingiliaji kati wa msaada wa kibinadamu w utoaji fedha ndio unaofadhiliwa kwa kiasi kidogo sana.