Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Griffiths akutana na waokoaji na familia zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi nchini Uturuki 

Mratibu wa misaada ya dharura wa UN Martin Griffiths akizuru Kahramanmaraş, Türkiye ambako amekutana na familia za waathirika wa matetemeko ya ardhi
OCHA
Mratibu wa misaada ya dharura wa UN Martin Griffiths akizuru Kahramanmaraş, Türkiye ambako amekutana na familia za waathirika wa matetemeko ya ardhi

Griffiths akutana na waokoaji na familia zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi nchini Uturuki 

Msaada wa Kibinadamu

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths, ambaye yuko ziarani nchini Uturuki, leo ametembelea mji wa Kahramanmaras, ulio karibu na kitovu cha tetemeko la ardhi nchini Uturuki. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, vitongoji vyote katika wilaya za kati za jiji vimeharibiwa kabisa, akiwa huko Bwana Griffiths amekutana na familia zilizoathiriwa na matetemeko hayo ambazo zimewekwa kwa katika kambi ya muda. 

Griffiths pia amezungumza na waokoaji wanaoendelea kufanya kazi katika maeneo yaliyoharibiwa.  

Amesema zaidi ya nchi 100 zimetuma timu za kukabiliana na hali hiyo ya dharura nchini Uturuki. 

Griffiths ameongeza kuwa “Timu za Umoja wa Mataifa pia ziko Kahramanmaras na kwingineko zikitoa msaada kwa timu za kimataifa za utafutaji na uokoaji wa manusura na ni operesheni kubwa zaidi ya kimataifa ya aina yake katika historia.” 

"Ujasiri wa watu wako, ujasiri wa wazazi wanaookoa familia zao na watoto kutoka kwenye vifusi, ujasiri wa waokoaji wako wanaofanya kazi saa 24 kwa siku kuwaondoa watu walionasa wakitarajia kusikia sauti nyingine, kupata mtu mwingine aliyeokoka hii inakufanya. usisahau ”, Griffiths amesema, akizungumza na waandishi wa habari. 

Mkuu wa misaada ya dharura wa UN Martin Griffiths amekutana na kiongozi wa timu ya uokozi ya Uturiuki Kahramanmaraş, Türkiye
OCHA
Mkuu wa misaada ya dharura wa UN Martin Griffiths amekutana na kiongozi wa timu ya uokozi ya Uturiuki Kahramanmaraş, Türkiye

Takriban wiki moja tangu matetemeko kutokea 

Siku sita zimepita tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria. Kama Jens Laerke, msemaji wa ofisi ya OCHA, alivyobainisha mapema wiki hii, "Kuna upenyo wa takriban siku saba  ambapo waathirika wanaweza kupatikana wakiwa hai."  

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, idadi ya vifo kutokana na tetemeko la ardhi tayari imefikia karibu watu elfu 26. 

Griffiths pia amehimiza kutosahau hatima ya wakimbizi nchini Uturuki, ambao, kutokana na matetemeko ya ardhi, walijikuta katika hali ngumu zaidi ya zahma mara mbili. 

Kesho Jumapili, Griffiths atasafiri hadi mpaka wa Uturuki na Syria na kuzuru kituo cha ukaguzi cha Bab al-Hawa, ambapo misaada ya kibinadamu iliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inawasilishwa katika mikoa iliyoathirika ya kaskazini-magharibi mwa Syria, ambayo iko chini ya udhibiti wa vikosi vya upinzani.