Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dkt. Tedros azindua ombi la kibinadamu kusaidia waathirika wa matetemeko Syria na Uturuki:WHO 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akikutana na Nour mtoto aliyepoteza wazazi wake wote kwenye tetemeko la ardhi Aleppo, Syria
WHO
Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akikutana na Nour mtoto aliyepoteza wazazi wake wote kwenye tetemeko la ardhi Aleppo, Syria

Dkt. Tedros azindua ombi la kibinadamu kusaidia waathirika wa matetemeko Syria na Uturuki:WHO 

Msaada wa Kibinadamu

Katika ziara yake nchini Syria, mkurugenzi mkuu wa Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO leo Jumapili amezindua ombi la kibinadamu la kukusanya dola milioni 43 kusaidia juhudi za kukabiliana na athari Syria na Uturuki baada ya matetemeko makubwa ya ardhi yaliyozikumba nchi hizo mbili wiki moja iliyopita na kusababisha vifo, watu kutawanywa na kujeruhi makumi ya maelfu ya watu. 

Ombi hilo limetolewa wakati mkurugenzi huyo mkuu Dkt, Tedros Adhanom Ghebreyesus alipofanya mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus baada ya kumaliza ziara yake mjini Aleppo kukagua maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi. 

Dkt. Tedros ameonyesha kuwa thamani ya msaada wa kibinadamu itaongezeka baada ya kubainika kwa kiwango cha maafa, akisisitiza haja ya kuongeza juhudi za kukabiliana na hali hiyo ili kufikia idadi kubwa ya watu walioathirika katika mikoa yote. 

Mkurugenzi huyo wa WHO amekaribisha kupunguzwa kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Syria na Marekani, huku akikaribisha idhini kamili ya hivi karibuni ya serikali ya Syria kuhusu misafara ya Umoja wa Mataifa katika mistari wa mbele wa migogoro, pamoja na hatua za kuongeza ufikiaji wa watu mpakani na amesema anatumaini kuwa hatua hiyo ingeendelea. 

Dkt. Tedros amesisitiza ahadi ya WHO "kuunga mkono watu wa Syria sasa na katika siku zijazo, wiki, miezi na miaka ili kukabiliana na janga hili na kujenga mfumo imara kwa Wasyria wote." 

WHO inatuma misaada ya vifaa vya matibabu  Syria kupika jeki kazi inayofanywa na mashirika ya misaada ya kibinadamu
WHO
WHO inatuma misaada ya vifaa vya matibabu Syria kupika jeki kazi inayofanywa na mashirika ya misaada ya kibinadamu

Tani za vifaa vya matibabu kwenda Syria 

WHO inatoa vifaa vya matibabu na kufanya kazi na washirika kutoa huduma maalum za matibabu, na hadi sasa imesambaza tani 110 za vifaa vya matibabu kwa maeneo yaliyoathirika kote Syria, kulingana na Dkt. Tedros. 

Leo jioni inatarajia kuwasili Damascus ndege iliyosheheni vifaa maalum na vya dharura vya matibabu ambavyo ni muhimu kwa wafanyikazi walio mstari wa mbele wanaposhughulikia majeruhi.  

Kwa kuongezea, shirika hilo limesema linaunga mkono uwezo wa timu maalum za matibabu zilizozko kwenye maeneo yaliyoathirika. 

Asubuhi ya tetemeko la ardhi, WHO mara moja ilipata fursa ya upatikanaji wa vifaa ambavyo vilikuwa vimewekwa hapo awali kaskazini-magharibi na Aleppo ili kuruhusu matibabu ya haraka ya watu waliojeruhiwa vibaya. 

Pongezi kwa ushujaa wa manusura na watoa misaada Syria 

Mkurugenzi wa WHO amesema ameona kwa macho yake athari mbaya za tetemeko la ardhi na kusikiliza hadithi za watu walionusurika, akibainisha kuwa alikutana Aleppo jana, Jumamosi, na mtoto Nour, ambaye alipoteza wazazi wake na amevunjika mkono wakati jengo lao la ghorofa sita lilipoanguka. 

Amesema Noor ni mfano mmoja tu wa janga linaloendelea kuathiri mamilioni ya watu.  

Ameashiria kwamba mzozo unazidi kuwa mbaya kutokana na migogoro, coronavirus">COVID-19, kipindupindu na kuzorota kwa uchumi, na sasa tetemeko la ardhi limeongeza athari isiyoelezeka. 

Kukiwa na watu milioni 26 walioathirika na matetemeko Syria na Uturuki dola milioni 42.79 zahitakia kukabiliana na hali ya dharura katika nchi zote mbili
WHO
Kukiwa na watu milioni 26 walioathirika na matetemeko Syria na Uturuki dola milioni 42.79 zahitakia kukabiliana na hali ya dharura katika nchi zote mbili

Ametoa shukrani zake za dhati kwa walionusurika na wahudumu wa kibinadamu, wakiwemo wafanyikazi wa WHO, akielezea kufurahishwa kwake na ukarimu, uhakika na matumaini yaliyoonyeshwa na manusura na kujitolea kwa washiriki wa msaada walio msitari wa mbele. 

Amesema WHO inasimama pamoja na watu wa Syria na Uturuki, na kubainisha kuwa mashirika ya kitaifa na kimataifa, majirani, misikiti, makanisa na makundi ya jumuiya yanaendesha mchakato wa kuwapatia watu chakula, maji safi, mahali pa kulala na kuwaweka salama na huduma za matibabu kwa majeruhi yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi, pamoja na kuwapa mahitaji mengine. 

Msaada zaidi wahitajika 

Hata hivyo Dkt. Tedros amesema misaada zaidi inahitajika. "Baada ya kuangalia usalama wa familia zao, wafanyikazi wetu walienda mara moja kwenye maghala kuanza kusambaza vifaa kwenye vituo vya afya. WHO inafanya kazi katika maeneo yote yaliyoathirika na kupanuka kote nchini, ikiwa ni pamoja na kaskazini magharibi. WHO mara moja ilitoa dola milioni 16 kutoka kwa mfuko wa dharura kukabiliana na hali za dharura nchini Syria na Uturuki.” 

Ameongeza kuwa anasubiri kuvuka mistari ya mbele ya migogoro kuelekea kaskazini-magharibi maeneo ambayo yameripotiwa kuathirika zaidi. 

Dk. Tedros amesema alikutana mapema Jumapili mchana na Rais Bashar al-Assad "ambaye alikuwa tayari kuhusu kuangalia sehemu za ziada za kuvuka mpaka ili kukabiliana na dharura hii.”