Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa ya Afrika yanaelekea katika kupunguza vifo vya ajali barabarani:UNECE/WHO

Misaa salama kwa waendesha baiskeli na watembea kwa miguu itasaidia Ethiopia kujikwamua vyema kupitia mradi wa pamoja unaofadhiliwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa usalama barabarni
UN-Habitat
Misaa salama kwa waendesha baiskeli na watembea kwa miguu itasaidia Ethiopia kujikwamua vyema kupitia mradi wa pamoja unaofadhiliwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa usalama barabarni

Mataifa ya Afrika yanaelekea katika kupunguza vifo vya ajali barabarani:UNECE/WHO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ajali za barabarani ndizo zinazoongoza kwa vifo vya vijana wa Kiafrika, hivyo serikali katika bara zima zimeazimia kuendesha magari katika mwelekeo mpya wa pamoja, katika Wiki ya kimataifa ya Usalama Barabarani, inayoadhimishwa kuanzia leo tarehe 15 hadi 21 Mei.

Takwimu mbaya za ajali za barabarani zinazoongezeka zimetoa msukumo wa kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na ajali mbili za basi nchini Senegal ambazo ziligharimu maisha ya watu 62 mwezi Januari.

Katika nchi Jirani ya Côte d’Ivoire, idadi ya kila siku ya vifo vya ajali mbaya za barabarani imeongezeka hadi 46, kutoka 12 mwaka 2012.

Katika kanda hiyo ya dunia ambayo imeaathirika zaidi na ajali za barabarani, kiwango cha vifo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ni watu 27 kwa kila watu 100,000.

Hiyo ni mara tatu zaidi ya wastani wa barani Ulaya wa watu tisa na zaidi ya wastani wa kimataifa wa watu 18, kulingana na tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa mataifa ya Ulaya (UNECE), ambayo inasimamia vyombo 59 vya kisheria vya shirika hilo kuhusu usafiri wa ndani, ikiwa ni pamoja na mikataba ya Umoja wa Mataifa ya usalama barabarani.

Kila mwaka, watu milioni 1.3 kote duniani hupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani, na mamilioni ya wengine hujeruhiwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO.

Magari yaliyobeba abiria kupita kiasi, usafiri wa bodaboda maarufu kama 'mshikaki' kama ilivyo pichani ni chanzo cha ajali nyingi.
Benki ya Dunia/Stephan Gladieu

Barani Afrika, vifo vya barabarani vinachangia takriban robo ya idadi ya waathiriwa wote wa ajali hizo duniani, ingawa bara hilo lina takriban asilimia 2 ya magari yote duniani, amesema mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani, Jean Todt, ambaye amerejea hivi karibuni kutoka kutembelea mitaa na barabara kuu za Afrika Magharibi.

Ameongeza kuwa "Afrika imeathiriwa zaidi na janga la ajali za barabarani ambazo ndio chanzo kikuu cha vifo vya vijana".

Wadau wanabadilisha gia

Akikutano na mamlaka na mashirika ya kiraia nchini Senegal na Côte d'Ivoire, Bwana Todt alisema uwekezaji mujarabu, unaweza kuokoa maisha.

Kwa sasa, serikali, sekta kibinafsi, na mashirika ya kiraia, kwa usaidizi wa mfuko wa Umoja wa Mataifa wa usalama barabarani, wanashirikiana katika mradi mpya ambao hatimaye unalenga kupunguza vifo vya ajali za barabarani na kuhakikisha usalama wa magari, imesema UNECE.

Mpango huo unasaidia kudhibiti usafirishaji na uagizaji wa magari yaliyotumika barani Afrika, hasa kuhusu kanuni na ukaguzi wa kiufundi.

Moja ya malengo ni kuagiza magari yaliyo salama na rafiki kwa mazingira barani Afrika ili kuepusha ajali mbayá za barabarani.

Huu ni mradi wa kwanza uliyowianishwa barani Afrika wa kudhibiti magari yaliyotumika kutoka nje, mradi huo utakapotekelezwa kikamilifu utakuwa na "athari kubwa chanya kwa mazingira, afya na usalama barabarani, limesema shirika hilo.

Nchi za Afrika zimejitolea kuimarisha utoaji wa taarifa kuhusu vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.
© UNICEF/Tanya Bindra
Nchi za Afrika zimejitolea kuimarisha utoaji wa taarifa kuhusu vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

Vifo vyazua kilio cha umma

Kando na matukio mabaya ya ajali za barabarani Senegal mwezi Januari, mwezi huo huo, huko Yamoussoukro, Côte d'Ivoire, ajali ya basi iliua watu 14 na kujeruhi wengine 70, wakati ajali nyingine ya magari kugongana kamam hiyo mwezi Agosti 2022 iliua watu 25 kaskazini mwa Abidjan.

Ajali hizi za mabasi zimeanika tatizo la kuchakaa kwa magari katika nchi zote mbili sambamba na ukosefu wa udhibiti wa kiufundi na kushindwa kuzingatia kanuni za barabara kuu, shirika hilo lilisema.

Kuzuia magari yasiyo salama

Kushughulikia magari kuukuu yaliyopitwa na wakati kunahitaji umakini maalum katika hasa Afrika Magharibi, imesema UNECE na kuongeza kuwa Senegal na Cote d'Ivoire zinategemea zaidi uagizaji wa magari yaliyotumika sana.

Mwaka 2016, wastani wa umri wa magari nchini Senegal ulikuwa miaka 18, na asilimia 40 zaidi ya miaka 20, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP).

Senegal ilikuwa imepitisha amri mwaka 2001 iliyoweka kikomo umri wa magari yanayoagizwa kutoka nje yasizidi miaka 5, na kuifanyia marekebisho mwaka wa 2012 hadi miaka 8, UNECE imesema.

Mzunguko wa umaskini

Juhudi pia zinafanywa kuwalinda watumiaji wa barabara walio hatarini zaidi, ambao ni watembea kwa miguu na waendesha baiskeli, ambao mara nyingi pia ndio maskini zaidi na wenye umri mdogo zaidi, shirika hilo limeripoti.

“Hakika, Afrika ina idadi kubwa zaidi ya vifo vya waendesha baiskeli na watembea kwa miguu, ambayo ni sawa na asilimia 44 ya jumla ya idadi ya vifo vyote vya barabarani.”

Mbali na janga la kibinadamu, ajali za barabarani huziingiza nchi katika mzunguko mbaya wa umaskini.

Kulingana na Benki ya Dunia, gharama ya ajali za barabarani inawakilisha asilimia 8 ya tato la taifa GDP la Senegal kwa mwaka na asilimia 7.8 ya pato la taifa la Côte d’Ivoire.

Barabara yenye msongamano Shenzhen, China.
Unsplash/Robert Bye
Barabara yenye msongamano Shenzhen, China.

Kukabiliana na leseni bandia kwa madereva walevi

“Kuendesha gari ukiwa umelewa, mwendo wa kasi, kusinzia, uzembe, kutotumia mikanda ya usalama na helmeti, na kutofuata kanuni za usalama barabarani ndio chanzo kikuu cha ajali za barabarani barani Afrika,” imesema UNECE.

Mambo mengine yaliyochangia “ni pamoja na kundi la magari chakavu katika usafiri wa umma, leseni bandia, ukosefu wa utekelezaji wa adhabu, na upungufu wa ukaguzi mkubwa wa kiufundi.”

Miongoni mwa masuluhu zitakazotekelezwa ni pamoja na haja ya kuimarisha huduma za afya kwa waathirika wa ajali, na kuzingatia mkataba wa Afrika wa usalama barabarani na mikataba ya msingi ya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani.

Kuongeza ufahamu pia kuna jukumu muhimu, UNECE ilisema.

Hatua Kali mpya

Kufuatia ajali mbaya mwezi Januari, Senegal ilitangaza hatua kali za kufanya barabara kuwa salama.

Hii ni pamoja na mpango wa kitaifa wa usalama barabarani, ukiwa na hatua 22 zinazolenga kupunguza idadi ya vifo na majeraha makubwa kwa angalau asilimia 50.

Hatua hizpo zinaanzia katika kuimarisha udhibiti wa barabara hadi kupunguza mzunguko wa magari ya usafiri wa umma.

Inamaanisha pia kupiga marufuku uingizaji wa matairi yaliyotumika, kutoa udhibiti wa kiufundi bila malipo huko Dakar kwa magari ya uchukuzi na bidhaa, na kufungua vituo vya udhibiti wa kiufundi kote nchini.

Kikosi cha kwanza cha polisi wa usalama barabarani

Nchini Côte d’Ivoire, mipango mipya inaimarisha sheria za usalama barabarani na kuunda kikosi cha polisi wa usalama barabarani.

Kufuatia ajali nyingi mbaya kaskazini mwa nchi, Serikali iliamua mwaka 2021 kutekeleza  sheria ya uvaaji wa kofia kwa waendesha baiskeli wote.

Ahadi zipo, iwe nchini Senegal au Côte d’Ivoire, UNECE inasema, na kuongeza kuwa kilichosalia ni sehemu ngumu zaidi ambayo ni utekelezaji na kupima maendeleo.