Hatua za kupambana na ajali za barabarani hazitoshi-WHO

Dizeli chafu zinachangia katika uharibifu wa hewa kupitia magari. Hapa ni  wachuuzi wakiuza bidhaa zao barabarani nchini Ghana
Jonathan Ernst/World Bank
Dizeli chafu zinachangia katika uharibifu wa hewa kupitia magari. Hapa ni wachuuzi wakiuza bidhaa zao barabarani nchini Ghana

Hatua za kupambana na ajali za barabarani hazitoshi-WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema hakuna hatua kubwa zilizopigwa katika kukabiliana na changamoto ya usalama barabarani kote duniani.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya WHO iliyozinduliwa leo mjini Geneva Uswis, vifo vitokanavyo na ajali za barabarani vinaendelea kuongezeka na kufikia vifo milioni 1.35 kwa mwaka.

Ripoti hiyo ambayo ni “Mtazamo wa kimataifa wa WHO kuhusu usalama barabarani 2018” inaeleza kwamba majeraha yatokanayo na ajali za barabarani sasa ndio chanzo kinachoongoza kwa vifo vya watoto na vijana wa kati ya umri wa miaka 5 hadi 29.

Akisisitiza haja ya kukabiliana na tatizo la ajali hizo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “Vifo hivi ni gharama isiyokubalika katika safari, hakuna kisingizio chochote kwa kutochukua hatua, hili ni tatizo ambalo lina suluhu. Ripoti hii ni wito kwa serikali na wadau wote kuchukua hatua zaidi kutekeleza mikakati hiyo.”

Ripoti hiyo pia imesema licha ya idadi ya vifo kuongeza , kiwango cha vifo kulingana na idadi ya watu duniani kinaonekana kutokuwa kikubwa sana kwa miaka ya karibuni, hii ikiaashiria kwamba juhudi zilizopo za usalama barabarani katika nchi za kipato cha wastani na kipato cha juu zimesaidia.

Naye balozi mwema wa kimataifa wa WHO kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza NCD na majeraha, Michael R Bloomberg amesema“Usalama barabarani ni suala ambalo halipatiwi uzito unaostahili na ni moja ya mambo ambayo yanatupa fursa kubwa ya kuokoa maisha koteulimwenguni. Tunafahamu ni hatua gani zinafanya kazi, será madhubuti na utekelezaji wake, miundo bora ya barabara na kampeni kubwa za uelewa kwa umma vinaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu katika miongo ijayo.”

Huduma za dharura baada ya ajali kutokea katika moja ya maeneo ya mji wa New  York, nchini Marekani. Huduma za haraka huokoa maisha lakini pia UN inataka hatua madhubuti kuzuia ajali hizo.
UN News/Vibhu Mishra
Huduma za dharura baada ya ajali kutokea katika moja ya maeneo ya mji wa New York, nchini Marekani. Huduma za haraka huokoa maisha lakini pia UN inataka hatua madhubuti kuzuia ajali hizo.


Ripoti imeongeza kuwa katika sehemu ambako hatua zimepigwa kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu ya será nzuri katika masuala ya hatari kama vile mwendo wa kasi kupita kiasi, kulewa na kuendesha ,magari, kutofunga mikanda , kutovaa helmeti kwa waendesha pikipiki, kutowalinda watoto, miundombinu salama kama kuwa na sehemu maalumu ya waendesha baiskeli na watembea kwa miguu, kuboresha viwango vya ubora wa magari ikiwemo breki na pia kuboresha huduma za baada ya ajali.

Kwani ripoti inasema hatua hizi zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na ajali za barabarani katika nchi 48 za kipato cha kati na za kipato cha juu. Hata hivyo imeonya kwamba hakuna hata nchi moja ya kipato cha chini iliyoonyesha kupunguza idadi ya vifo kwa ujumla na kwa asilimia kubwa ni kwa sababu hatua hizi zinakosekana.

Kwa mantiki hiyo ripoti inasema “hatari ya vifo vya ajali za barabarani katika nchi za kipato cha chini ni mara tatu zaidi ya ilivyo katika nchi za kipato cha juu, na viwango hivyo ni vikubwa zaidi barani Afrika ambapo ni uwiano wa watu 26.6 kwa kila watu 100,000 na kiwango kidogo zaidi ni barani Ulaya ambako ni uwiano wa watu 9.3 kwa kila watu 100,000.”

Tangu kutolewa kwa ripoti iliyopita hadi sasa kanda tatu zimeorodhesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani ambazo ni Amerika, Ulaya na Pacific Magharibi. Ripoti inasema tofauti za vifo vya ajali za barabarani zinaonekana pia katika aina ya watumiaji wa barabara .

Ajali za barabarani yatajwa kuwa sababu kuu ya vifo vya vijana
UN News
Ajali za barabarani yatajwa kuwa sababu kuu ya vifo vya vijana

 

Kimataifa waendesha baiskeli na watembea kwa miguu ni asilimia 26 ya vifo vyote huku Afrika pekee ikichukua asilimia 44 ya vifo hivyo ikifuatiwa na Metiterrania Mashariki asilimia 36.  Waendesha pikipiki na abiria kwenye magari ni asilimia 28 ya vifo vyote vya ajali barabarani na asilimia kubwa ya vifo hivi iko Kusini Mashariki mwa Asia ikiwa ni asilimia 43 ikifuatiwa na Pacific Magharibi asilimia 36.