Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi yaanza kutoa chanjo ya homa ya matumbo

Mhudumu wa afya nchini Malawi akipatia mtoto matone ya vitamin A.
UNICEF Malawi
Mhudumu wa afya nchini Malawi akipatia mtoto matone ya vitamin A.

Malawi yaanza kutoa chanjo ya homa ya matumbo

Afya

Kwa msaada kutoka Ubia wa Chanjo duniani, GAVI, na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la Afya duniani, WHO na lile lakuhudumia watoto,UNICEF na wadau wengine, serikali ya Malawi hii leo imezindua kampeni ya kitaifa ya wiki moja ya kutoa chanjo dhidi ya surua, rubella na homa ya matumbo, kampeni yenye lengo za kuziba pengo la chanjo.

Taarifa iliyotolewa hii leo na WHO kutoka Lilongwe, Malawi na Geneva, USwisi inasema kampeni hiyo iliyozinduliwa leo itahusisha pia watoto kupatiwa chanjo dhidi ya polio pamoja na matone ya vitamin A na itafuatiwa na ujumuishaji wa chanjo dhidi ya homa ya matumbo kwenye programu za utoaji chanjo.

Watoto milioni 9 ndio walengwa

Zaidi ya watoto milioni 9 wenye umri wa hadi miaka 15 watanufaika na kampeni hii yenye lengo la kuzuia milipuko ya surua na magonjwa mengine, na vile vile kuimarisha kinga ya mwili kwa watoto.

WHO inasema chanjo dhidi ya homa ya matumbo, TCV itatolewa kwa dozi moja na kwamba “chanjo hizo zitatolewa kupitia vituo vya afya, halikadhalika watoa huduma watatumia magari kufikia walengwa ambako wako maeneo ya ndani zaidi.”

Taarifa hiyo imesema baada ya kumalizika kwa kampeni hiyo ya wiki moja, chanjo dhidi ya homa ya matumbo itajumuishwa kwenye ratiba ya chanjo, ikipatikana kwenye vituo vya afya kwenye wilaya zote nchini Malawi na watoto wanapotimiza miezi 9 watapatiwa pamoja chanjo ya surua.

Akizungumzia hatua hii, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema “hii ni hatua muhimu kwa Malawi. Watoto wako hatarini kupata magonjwa yanayohusiana na homa ya matumbo. Kufanikiwa kujumuisha chanjo hii kwenye programu ya utoaji chanjo kutachangia kupunguza mzigo wa homa ya matumbo Malawi.”

WHO inasema nchi mara nyingi huendesha kampeni za kuziba pengo ili kuimarisha utoaji wa chanjo na kufikia wale ambao walikosa kutokana na dharura, mathalani kwa Malawi kimbunga Freddy na milipuko ya polio na kipindupindu.

Homa ya matumbo husababishwa na nini?

Ugonjwa wa homa ya matumbo ujulikanao pia kama kuhara damu husababishwa na kimelea au bakteria Salmonella Typhi, na husababisha vifo.

Mwaka 2019, zaidi ya wagonjwa milioni 9 wa homa ya matumbo waliripotiwa Malawi na kati yao zaidi ya 110,000 walifariki d unia.

Ugonjwa huu husababishwa na kula chakula au kunywa maji machafu, ikimanisha kwamba mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili na ukimbizi hutumbukiza jamii kwenye hatari ya kupata maambukizi ya homa ya matumbo.

Chanjo ni jawabu kwani dawa ina usugu

Chanjo dhidi ya homa ya matumbo iliidhinishwa na WHO mwaka 2018 na ina ufanisi mkubwa katika kuzuia ugonjwa huo na wanaweza kupatiwa watoto kuanzia wenye umri wa miezi 6 na kuendelea.

Nchini Malawi ugonjwa huu hupatikana mara kwa mara na chanjo imethibitisha kuwa na ufanisi wakati huu ambapo tiba dhidi yake imekumbwa na kigingi kutokana na usugu wa dawa.

Malawi inakuwa nchi ya 6 duniani na ya 3 barani Afrika kujumuisha TCV kwenye programu ya chanjo. Nchi zingine zilizojumuisha chanjo hiyo ni pamoja na Pakistan, Liberia, Zimbabwe na Nepal.