Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO Tanzania yachukua hatua kukwamua wavuvi wanawake na wanaume kupitia FISH4ACP

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO nchini Tanzania limeendesha warsha ya siku 2 kwenye mkoa wa Kigoma ulioko magharibi mwa taifa hilo kuwapatia wadau matokeo ya utafiti wa jinsi ya kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye sekta ya uvuvi.
Idhaa ya UN
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO nchini Tanzania limeendesha warsha ya siku 2 kwenye mkoa wa Kigoma ulioko magharibi mwa taifa hilo kuwapatia wadau matokeo ya utafiti wa jinsi ya kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye sekta ya uvuvi.

FAO Tanzania yachukua hatua kukwamua wavuvi wanawake na wanaume kupitia FISH4ACP

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO kupitia  mradi  wake  FISH4ACP  limepokea matokeo ya Utafiti kuhusu Usawa wa Kinjisia katika Masuala ya Uvuvi, moja ya hoja ambayo ikitekelezwa vema itasaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs hasa la kutokomeza njaa na kuondokana na umaskini.

Uzinduzi wa matokeo hayo umefanyika wakati wa kikao cha siku mbili  hapa mkoani Kigoma na unatoka na Utafiti kuhusu Usawa wa kijinsia katika mnyororo wa thamani wa mazao ya Uvuvi Ziwa Tanganyika ukishirikisha wadau mbalimbali  wakiwemo wavuvi, wachakataji, wasafarishaji,  Jeshi la Polisi, serikali na wadau wa maendeleo.

Devotha Songorwa wa Redio washirika Kids Time FM nchini Tanzania ndio shuhuda wetu wa uzinduzi huo uliofanyika katika  Mkoa wa Kigoma, Magharibi mwa Taifa hilo la Afrika Mashariki amezungumza na Afisa Mtaalamu Mnyororo wa Thamani wa Uvuvi na Ufugaji  Viumbe Maji, kutoka FAO nchini Tanzania anayesimamia mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma nchini Tanzania, Hashim Muumin,  ambaye amempatia muhtasari wa matokeo ya utafiti huo kutokana na mradi huo wa miaka mitano  unaotekelezwa katika nchi 12 za Afrika  ikiwemo  Tanzania .

“Imeonekana uvuvi ni suala la kiume zaidi kuliko wanawake lakini kwa utafiti tulioufanya tuliona asilimia 78 ya wachakataji ni wanawake na  asilimia  99 ya wavuvi ni wanaume na kuna masuala ambayo yanawakwaza kina wanawake na wanaume wavuvi katika kujikwamua kiuchumi,” amesema Afisa huyo.

Ameeleza kuwa  utafiti huo utasaidia kubaini changamoto zinazokabili masuala ya Jinsia na fursa zake  katka Ziwa Tanganyika ili kutoa mwamko kwa wanawake na watu wenye ulemavu kujihusisha na Uvuvi kuinua kipato chao.

“Shirika la FAO limeanzisha dawati la jinsia katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambalo linafanya kazi na sisi kama mradi wa FISH4ACP tunafanya kazi kwa karibu sana kuhakikisha sera, mikakati na sheria za Serikali zinatekelezwa,” amebainisha Hashim.